Mtibwa yachemsha kwao, yapigwa na Lipuli 2-1

Wednesday May 16 2018

 

By Mwandishi Wetu

Kikosi cha Mtibwa Sugar kimeshindwa kutamba kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Manungu Complex mkoani Morogoro baada ya kufungwa na Lipuli FC mabao 2-1.
Seif Abdallah 'Karie' ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo, ndiye aliyeifungia Lipuli mabao yote mawili dakika 16 na 71 wakati Mtibwa wao, walipata bao la kufutia machozi dakika 53 kupitia kwa Rifat Khamis .
Katika mchezo huo ambao timu hizo zilimpa heshima beki wa kushoto wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Alphonce Modest mwenye matatizo ya miguu, kabla ya mchezo aliingizwa uwanjani sambamba na kupiga picha na wachezaji.
Timu zote zilicheza kwa kushambuliana na dakika ya 76, Mtibwa ambao ni maarufu kwa jina la Wakatamiwa walipata pigo kwa  mlinda mlango wao, Benedict Tinocco kuonyeshwa kadi nyekundu. Kutokana na tukio hilo Mtibwa walilazimika kumtoa Ramadhan Kihimbwa na nafasi yake ikachukuliwa na Shaaban Hassan 'Kado' aliyekwenda kukaa golini.