Mtibwa Sugar kuijipima kwa Lipuli

Dar es Salaam. Mtibwa Sugar  inakwenda  mkoani Iringa kesho Jumamosi tayari kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Lipuli  utakaofanyika  Jumapili  kwenye Uwanja wa Samora Iringa.

Timu hiyo inakwenda kwenye mchezo huo bila  kipa wake namba moja Shaban Kado ambaye yupo  Dar es Salaam akiendelea na matibabu ya  mguu baada ya kuumia katika mchezo uliopita wa  kirafiki dhidi ya Simba.

Msemaji wa Mtibwa Sugar,Thobias Kifaru  alisema  wamepata mwaliko kutoka kwa Lipuli ambao Jumapili wanazindua jezi zao watakazotumia kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi.

"Lipuli wameomba kucheza na sisi na tumeona ni  nafasi nzuri kwa timu yetu kucheza mchezo huo  kwa ajili ya maandalzi ya ligi ambayo karibu  inaanza, hivyo utatusaidia kukijenga kikosi  chetu.

"Wachezaji wote watasafiri kwenda Iringa  isipokuwa kipa Shaban Kado na mshambuliaji Stamil Mbonde ambao wanaendelea na  matibabu na tunawaombea warejee mapema  kabla ya ligi kuanza," alisema Kifaru.

Mtibwa Sugar imeonekana kuwa itakuwa moja  ya timu tishio msimu ujao kutokana na usajili iliofanya  licha ya kuondokewa na wachezaji  wengi wa kikosi cha kwanza.

Timu hiyo imewasajili Shaban Kado,Riphat  Hamis, Hassan Isihaka, Salum Kanoni, Kelvin Sabato, Hassan Dilunga, Hussei  Iddi  na Salum Ramadhani.

Mtibwa Sugar itafungua Ligi Kuu Bara  Agosti 26 kwa kucheza na Stand United  kwenye Uwanja wa Manungu Turiani, Morogoro.