Mtanzania awakamata akili makocha NBA

Dar es Salaam. Mchezaji chipukizi wa mpira wa kikapu Jesca Ngisaise, amekuwa kivutio kwa makocha wa Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA).

Jesca alionyesha kiwango bora alipokuwa kambini Afrika Kusini akiwa miongoni mwa wachezaji 80 kutoka Afrika walioshiriki mafunzo ya mpira wa kikapu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha wa mpira wa kikapu Bahati Mgunda, alisema chipukizi huyo alifanya vyema katika mafunzo hayo na kuwavutia baadhi ya makocha na wachezaji wa Ligi Kuu Marekani.

Mgunda ambaye ni kocha wa timu ya Taifa ya vijana alisema kipaji, uwezo na kujituma kulimpa fursa mchezaji huyo kuchaguliwa katika kikosi cha ‘All Stars’.

“Jesca anatakiwa kuzingatia mafunzo aliyokuwa akipewa Afrika Kusini, ni mchezaji ambaye ana uwezo mkubwa wa kuitangaza Tanzania kupitia mpira wa kikapu,” alisema Mgunda aliyekuwa kocha msaidizi katika mafunzo hayo.

Awali, Jesca ambaye ni mchezaji wa timu ya Ukonga Queens, alisema hatabweteka na mafanikio aliyopata Afrika Kusini kwa kuwa lengo lake ni kucheza mpira wa kikapu katika mashindano ya Ligi Kuu Marekani.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) Phares Magesa alisema wachezaji ambao watakuwa wakifanya vyema katika mafunzo watapelekwa NBA Akademi au timu zinazocheza Ligi ya NCAA Marekani