Mtanzania atamba mpira wa meza Kenya

Muktasari:

Sara ameiwakilishi shule ya Aga Khan Academy Mombasa amekuwa miongoni mwa wachezaji watatu kutoka wilaya ya Mvita kupata kuwakilisha katika mashindano hayo mkoa.

Dar es Salaam. Mchezaji wa mpira meza wa Tanzania, Sara Alidina amefuzu kucheza mashindano ya mikoa ya Kenya iliyopangwa kuanza wiki ijayo baada ya kushika nafasi ya pili katika hatua ya awali.

Sara ameiwakilishi shule ya Aga Khan Academy Mombasa amekuwa miongoni mwa wachezaji watatu kutoka wilaya ya Mvita kupata kuwakilisha katika mashindano hayo mkoa.

Mtanzania huyo alianza michuano hiyo kwa vishindo baada ya kumchapa Rachel Thomas kwa seti 2-0 (11-4, 11-6) na baadaye kupata ushindani mgumu kutoka kwa Elizabeth Ochieng ambaye alianza kwa kushinda kwa 15-14 kabla ya kumbadilishia kibao na kuibuka na ushindi kwa seti mbili zilizobaki kwa  11-5 na 11-4).

Sara aliendelea kutamba katika mashindano kwa kumchapa  Christine Augustine kwa 2-0 (11-4, 11-6) na baadaye kushinda dhidi ya Maliha Haji kwa  2-0 (11-4, 11-5) na kupoteza kwa 2-0 dhidi ya Rachel Simon kwa 8-11 na 9-11.

Pamoja na kushindwa dhidi ya Rechal, Sara alifuzu hatua ya robo fainali na kushinda mechi dhidi ya Eliza Wanjiru kwa  2-0 (11-4, 11-4) na kushinda tena kwa 2-0 katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Catherine Okoth  kwa 11-4 na 11-6. Hata hivyo alikumbana na kigindi katika fainali kwa kufungwa 2-1 dhidi ya Krupa Vyas kwa 11-8, 9-11 na 11-7.

Sara alisema mashindano hayo yalikuwa magumu na kushukuru Mungu kwa kufuzu hatua ya mashindano ya mikoa.

“Lengo ni kutwaa ubingwa pamoja na kupata ushindani mkubwa, mechi nyingi zilikuwa ngumu na hasa ukingatia kuwa nacheza na wachezaji wakubwa zaidi yangu. Hii imesababisha kuchoka na kufungwa katika hatua ya fainali,” alisema Sara.