Msuva kusaka ushindi Algeria

Muktasari:

  • Difaa ilisafiri Ijumaa ya wiki iliyopita kutoka Morocco hadi Algeria ambako itacheza kwa mara ya pili katika nchi hiyo huku ukiwa ni mchezo wa tatu kwenye hatua ya makundi.

MSHAMBULIAJI wa Difaa El Jadida, Saimon Msuva amesema wanahitaji matokeo ya ushindi kwenye mchezo wao wa kesho dhidi ya ES Setif ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuingia mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Difaa ilisafiri Ijumaa ya wiki iliyopita kutoka Morocco hadi Algeria ambako itacheza kwa mara ya pili katika nchi hiyo huku ukiwa ni mchezo wa tatu kwenye hatua ya makundi.

Awali timu anayoichezea Msuva ilicheza mchezo wake wa kwanza Algeria dhidi ya MC Alger, Mei 4 mwaka huu na kutoka sare ya bao 1-1.

“Ushindi utaweka hai matumaini yetu ya kucheza mtoano kwa upande wa maandalizi yetu ni mazuri kwa jumla, tumesafiri salama na hakuna fitna zozote ambazo tumekutana nazo labla kwa sababu zote hizi ni timu za Kiarabu.

“Nategemea mchezo kuwa mgumu maana wapinzani wetu nao watahitaji kutumia uwanja wao wa nyumbani vizuri,” alisema mshambuliaji huyo.

Msuva aliyeifungia Difaa mabao 11 msimu uliopita wa Batola Pro, anategemewa na kocha wa kikosi hicho, Abderrahim Taleb kuingoza timu kwenye safu ya ushambuliaji.

Difaa ambayo ipo Kundi B nafasi ya tatu na pointi moja itacheza mchezo huo bila ya aliyekuwa pacha wa Msuva kwenye safu ya ushambuliaji, Hamid Ahadad ambaye amejiunga na Zamalek ya Misri.

Kinara anayeongoza msimamo wa Kundi B ni TP Mazembe ya DR Congo yenye pointi sita, inayofuata ni MC Alger ikiwa na pointi nne, ES Setif ndiyo vibonde kundi hilo ikishika mkia bila pointi.