Msuva atupia Difaa yaua Morocco

Muktasari:

  • Msimu uliopita Mtanzania huyo alifunga mabao 11, katika ligi ya Batola Pro

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Difaa El Jadida, Saimon Msuva ameendeleza moto wake wa kuzifumania nyavu baada ya kufunga bao mmoja timu yake ikishinda 2-1 dhidi ya Olympique Club de Khouribga katika Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’.

Baada ya kuukosa mchezo wa kwanza wa msimu dhidi ya FAR Rabat kutokana na majukumu aliyokuwa nayo ya kuitumikia Taifa Stars, Msuva aliongoza Difaa jana kwenye mchezo ambao wameibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Msuva alifunga bao lake la kwanza la msimu wa 2018/19 dakika ya 83 ambalo liliihakikishia ushindi timu yake  wa mabao 2 mbele ya Khouribga kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Ben Ahmed El Abdi.

Bao la kwanza la Difaa kwenye mchezo huo, lilifungwa na Karim al-Hashemi dakika ya 74 huku lile la kufutia machozi kwa Khouribga likifungwa na Youssef Oggadi dakika 90.

Difaa inaongoza msimamo wa Batola Pro, kufuatia kuvuna kwao pointi sita kwenye michezo miwili, FUS Rabat inafuata nafasi ya pili ikiwa na pointi nne.

Huu ni msimu wa pili kwa Msuva kuichezea Difaa, msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na kuwa mchezaji wa kigeni aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye Batola Pro.