Msuva aibeba Difaa Ligi ya Mabingwa Afrika

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo tayari amefunga mabao manne katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu

 Mshambuliaji wa Kitanzania na Difaa El Jadida, Saimon Msuva amesema anafuraha kubwa baada ya kumalizika mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital ya DR Congo.

Msuva ameiongoza Difaa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo makubwa Afrika kwa ngazi ya klabu baada ya kutoka kwao sare ya mabao 2-2 katika mchezo huo wa marudiano, Congo hivyo kutinga kwa jumla ya mabao 3-2.

Katika mchezo wa kwanza iliofanyika Morocco, Difaa ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Msuva.

Katika mchezo wa marudiano Msuva hakuanza katika kikosi cha kwanza aliingia na kuchangia upatikanaji wa bao la kusawazisha kwa kupiga pasi ya mwisho ndani ya dakika nne za nyongeza.

 "Mungu ni mwema. Ile ishara ya kuonyesha vidole vyangu juu nilimaanisha hivyo, nimefurahi sana kwa sababu mchezo ulikuwa ngumu na jamaa walicheza vizuri kwa kutushambulia sana lakini uzuri tulikuwa na akiba ya bao moja kwa hiyo hata kama tungefungwa 2-1 bado tulikuwa na nafasi, " alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga anategemea kujiunga na Taifa Stars nchini Algeria kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao, Machi 22.

"Wasingeweza kunipa ruhusa ya kuondoka na kuja Tanzania  moja kwa moja baada ya mechi, kwa sababu ya Kalenda ya FIFA kuanza kuhesabiwa Machi 19 na ndiyo siku ambayo nasikia walisafiri, " alisema Msuva mwenye mabao 6 kwenye Ligi ya Morocco.

Nyota wengine wa Taifa Stars ambao wanategemewa kujiunga na timu hiyo nchini Algeria ni Shomari Kapombe, Shiza Kichuya, Aishi Manula, Erasto Nyoni wa Simba ambao walikuwa nchini Misri kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Al Masry.

Pia, nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta ambaye anatokea Ubelgiji kwenye klabu yake ya KRC Genk pamoja na Rashid Mandawa wa BDF IX ya Botswana.