Msuva aisubili kwa hamu safari ya Morocco

Muktasari:

  • Msuva ataondoka nchini kesho usiku kuelekea Morocco ili kukamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo maarufa kama ‘Botola’, Usajili huo unatajwa kuigharimu timu hiyo zaidi ya Sh 300 milioni.

Winga wa Yanga, Simon Msuva amejawa na furaha kufuatia akijiandaa safari yake ya kwenda kujiunga na  Difaa Hassani d'el-Jadida, Morocco.

Msuva ataondoka nchini kesho usiku kuelekea Morocco ili kukamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo maarufa kama ‘Botola’, Usajili huo unatajwa kuigharimu timu hiyo zaidi ya Sh 300 milioni.

 “Kama siyo kusafiri kwenda Rwanda nadhani ningekuwa tayari Morocco, lakini hakuna kilicho halibika  maana kesho rasmi nitaondoka kuelekea nchini humo ili kumalizana nao.

“Huwa naamini kila kitu  kinafanyika kwa wakati, nilifanikiwa kufanya vizuri nchini kwa maana ya Ligi Kuu, sasa huu ni muda wa kufanya vizuri katika ngazi nyingine  ya mpira, ujue hata Samatta naye alitoka Simba na kwenda TP Mazembe.

“Hakuna linaloshindikana, asanteni ndugu zangu wa Yanga ambao tumeishi kwa pamoja bila matatizo yoyote na kwa moyo mmoja mmeniruhusu nikapiganie mafanikio, nawatakia mafanikio mema kuelekea msimu mpya wa VPL.” alisema winga huyo.

Msuva aliongeza kwa kusema amejipanga kukabiliana na changamoto mpya ndani ya timu hiyo ikiwemo kupigania nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo.