Msuva adatisha Wazungu, dau lake kufuru tupu

Muktasari:

Unaambiwa dau lake sokoni kwa sasa ni kufuru na hakuna klabu ya Tanzania inaweza kumnunua tena, hata Azam ambayo bosi wake ana pesa kama mchanga.

STAA wa Tanzania, Simon Msuva amezidi kunoga. Kiwango chake kwenye klabu ya Difaa Al Jadida ya Morocco kimewapagawisha Wazungu na sasa wameanza kudata kabisa na mavitu yake.

Unaambiwa dau lake sokoni kwa sasa ni kufuru na hakuna klabu ya Tanzania inaweza kumnunua tena, hata Azam ambayo bosi wake ana pesa kama mchanga.

Kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt, thamani ya Msuva sokoni kwa sasa ni Pauni 428,000 (Sh 1.36 bilioni).

Hilo ni ongezeko mara nne ya fedha ambazo Yanga ilimuuza kwenda Jadida katikati ya mwaka jana.

Dau hilo linamfanya Msuva kuwa mchezaji namba mbili nchini kwa thamani kubwa baada ya Mbwana Samatta.

Huwezi kuamini kwa mujibu wa mtandao huo, hadi winga mwenye nguvu na kasi, Thomas Ulimwengu anasubiri kwani kwa sasa thamani yake sokoni ni Pauni 90,000 (Sh286 milioni).

Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji ndiye anawa-kimbiza nyota wote nchini kwani thamani yake kwa sasa ni Pauni 2.7 milioni sawa na Sh8.5 bilioni.

Beki wa Baroka FC, Abdi Banda anashika namba tatu kwa thamani kubwa nchini na mtandao huo wa Transfermarkt unamtaja kuwa ana thamani ya Pauni 271 (Sh858 milioni).

AKIMBIZA MOROCCO

Kupanda kwa thamani ya Msuva kwa kasi kumechagizwa kiasi kikubwa na uwezo wake wa kutengeneza nafasi na kufunga kwenye Ligi Kuu Morocco.

Mpaka sasa Msuva anashika namba tano kwenye chati ya wafungaji bora wa Ligi ya Morocco maarufu kwa jina la Batola Pro akiwa na mabao sita. Kinara wa mabao wa ligi hiyo ni Mouhcine Iajour wa Raja Casablanca aliyefunga mara 14.

Licha ya kufunga mabao sita, Msuva ndiye mchezaji wa kigeni anayeongoza kwa kufunga zaidi kwenye ligi hiyo yenye ushindani mkubwa barani Afrika, akifuatiwa na straika Mfaransa, Saer Sene anayekipiga Chabab Atlas Khenifra ambaye ana mabao matano.

HUKO CAF NDIO BALAA

Msuva wa sasa unaambiwa ni wa kimataifa na kasi yake kwenye michuano ya CAF ya Ligi ya Mabingwa Afrika imeibeba timu yake na kufikisha hatua ya makundi.

Msuva tayari amefunga mabao manne kwenye ligi hiyo ikiwamo Hat Trick aliyofunga kwenye mchezo wa kwanza tu dhidi ya Benfica Bissau.

Pamoja na kufunga mabao hayo, Msuva alifanya kazi kubwa kwenye mechi mbili dhidi ya AS Vita ya DR Congo ambapo alifunga bao pekee la ushindi nyumbani kisha akatoa pasi ya bao la kusawazisha kwenye mechi ya marudiano ugenini ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

MABAO TAIFA STARS

Tangu Msuva atue Morocco ni kama vile nyota ya Samatta imefifia kwani winga huyo amekuwa ndiye staa mkubwa wa Taifa Stars kwa sasa.

Mara tu baada ya kutua Morocco, Msuva aliitwa kuichezea Stars dhidi ya Botswana na alifunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa 2-0.

Msuva akaitwa tena kwenye mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Malawi akatupia bao moja tena maridadi la kona ya moja kwa moja akimlipa Shiza Kichuya aliyewahi kufunga bao kama hilo kwenye mechi ya watani wa jadi dhidi ya Yanga.

Msuva amefikisha bao lake la nne kwa Stars tangu atue Morocco, juzi Alhamisi dhidi ya Algeria, ikiwa ni bao la kufutia machozi kutokana na kipigo cha mabao 4-1 ilichopokea timu hiyo ya Taifa.

AACHA REKODI YANGA

Msuva mbali na kucheza Morocco kwa sasa, ameacha rekodi kibao tamu kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga.

Mojawapo ni kuifungia Yanga jumla ya mabao 62 katika mechi za Ligi Kuu Bara kwa misimu mitano tangu msimu wa 2012-2017.

Pia hadi anaondoka Yanga alikuwa akilipwa Sh4 milioni na kuwa mchezaji mzawa anayelipwa zaidi ndani ya klabu hiyo.

Vilevile aliondoka Yanga akiwa na rekodi ya kushinda mataji manne ya Ligi Kuu Bara, matatu ya Ngao ya Hisani na moja la FA.

Msuva pia alishinda tuzo ya mfungaji bora wa Lig Kuu Bara mara mbili tofauti pamoja na kuwa mchezaji bora wa msimu mara moja.

Rekodi hizo zinamfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wachache waliopita Yanga ambao wamepata mafanikio makubwa.