Msimbazi wajitosa kwa beki wawa

Muktasari:

  • Raia huyo raia wa Ivory Coast aliyekuwa akicheza El Merreikh ya Sudan, amekuwa akifanya mawasiliano na vigogo wa Simba na Yanga ili arudi kukipiga na moja ya klabu hizo, lakini ikionekana Simba wakimpigia hesabu kali, huku Yanga nao wakimwinda lakini wote wakitaka aje ajarabiwe kwanza.

BEKI kisiki wa zamani wa Azam, Pascal Wawa mpaka sasa bado hajajua hatma yake iwapo atarudi tena kucheza soka Tanzania au la, baada ya dili lake la kutua Jangwani kudaiwa kuingizwa mikono na Wekundu wa Msimbazi.

Raia huyo raia wa Ivory Coast aliyekuwa akicheza El Merreikh ya Sudan, amekuwa akifanya mawasiliano na vigogo wa Simba na Yanga ili arudi kukipiga na moja ya klabu hizo, lakini ikionekana Simba wakimpigia hesabu kali, huku Yanga nao wakimwinda lakini wote wakitaka aje ajarabiwe kwanza.

Mwanaspoti linafahamu Wawa amekuwa akifanya mawasiliano na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ na wapo katika hatua nzuri, ila kinachokwamisha dili lake ni maafikiano ya masilahi.

Inaelezwa Wawa na beki wa zamani wa Gor Mahia, Mkenya Musa Mohammed wapo kwenye rada za mabosi wa Msimbazi, lakini mwafaka wa masilahi bado haujafikiwa hasa kutokana na ukweli beki huyo ana muda mrefu hajacheza mashindano makubwa.

Anasema wote walifanya nao mazungumzo na wamefikia katika hatua nzuri lakini kinachowakwamisha kwa Wawa hajacheza muda mrefu mashindano na kumwambia aje afanye kwanza majaribio ambalo naona hataki kulikubali mpaka sasa.

“Kama Wawa atakataa kufanya majaribio tutaachana naye. Tunaogopa huenda akawa na majeraha ya muda mrefu na tukashindwa kumtumia, ila kwa Musa hatuna wasiwasi nae kwani yupo vizuri na yupo katika hatua nzuri,” kilisema chanzo kutoka Simba.

YANGA NAO HAWA

Upande mwingine, licha ya Simba kuonekana kumfukuzia Wawa, sio kwamba Yanga wamesalimu amri, ila wanashindwana kwenye suala la masilahi tu, pia wanataka aje kwanza kufanyiwa majaribio na Kocha Mwinyi Zahera.

Iko hivi. Kamati ya usajili ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Hussen Nyika walifanya mazungumzo na Wawa na kufikia katika hatua nzuri ambayo wangeweza kukamilisha usajili wake, lakini wakashindwa kumtumia tiketi mpaka leo hii.

Nyika aliweka bayana aliyekwamisha dili ya Wawa ni Kocha Zahera aliyetaka kwanza kuwaona wachezaji kabla ya kusainishwa kwa lengo la kutaka kuwa na kikosi bora na chenye uwezo wa kuipigania Yanga katika mashindano ya aina yoyote.

“Unajua Wawa ni mchezaji mzuri na kuna watu katika kamati yangu walipendekeza asajiliwe kuongeza nguvu kikosini, hata hivyo, mtu wa mwisho kuamua hatma yake ni Kocha Zahera ambaye amesema asisajiliwe mtu mpaka arudi kuwaona mwenyewe.”

“Tunayo majina ya wachezaji wa kigeni kutoa nje ya nchi ambao kocha alipendekeza, lakini Wawa hayumo ndio maana alisema kama ni mzuri ni mpaka amwone kwa kumjaribu ndipo aamue atue Yanga ama la,” alisema Nyika.