Mrwanda Alliance kachimba mkwara

KOCHA Mkuu wa Alliance FC, Kayiranga Baptiste amesema mkakati wake ni kuiandaa timu kiushindani ili kuwania nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu msimu ujao.

Kayiranga ambaye ni raia wa Rwanda anatarajia kukiongoza kikosi hicho cha jijini Mwanza ambacho kitashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.

Akizungumza baada ya mazoezi juzi katika Uwanja wa Kirumba, kocha huyo alisema mkakati wake ni kuiandaa timu kiushindani na kushika nafasi tatu za juu.

Alisema hii ni mara yake ya kwanza kufanya kazi hapa nchini na havijui klabu zote, hivyo hata iwe Simba au Yanga zisitarajie mteremko kwa Alliance iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

“Mkakati wangu ni kuiandaa timu kiushindani, hii ni mara yangu ya kwanza kufanya kazi hapa Tanzania, sizijui Simba wala Yanga kwa undani lakini najua ni timu kubwa zinashiriki mashindano kimataifa, lakini zisitarajie mteremko,” alisema Kayiranga.

Mnyarwanda huyo aliongeza suala la usajili tayari amewasilisha mapendekezo yake kwenye uongozi hivyo anasubiri utekelezaji na kwa sasa anaendelea na mazoezi na waliopo.

Alisema anaamini ligi itakuwa na ushindani kutokana na kila timu kujiandaa na kutokana na uzoefu wake timu itafanya vizuri.

“Nimewasilisha ripoti na ushauri wa benchi la ufundi kwa viongozi, kwa sababu tunaelekea kwenye soka la ushindani, kwa hiyo nasubiri utekelezaji wakati huo tunaendelea na mazoezi na hawa waliopo,” alisema kocha huyo.