Mourinho na panga pangua Man United

Muktasari:

Baada ya Louis van Gaal kushindwa kuwafufua tangu David Moyes aliyemrithi Sir Alex Ferguson kushindwa kufanya hivyo, mambo yamekuwa mchanganyiko Old Trafford.

MANCHESTER United bado wanaelekea kuwa katika kipindi cha mpito, ambapo kocha wao, Jose Mourinho anaweka mikakati.

Baada ya Louis van Gaal kushindwa kuwafufua tangu David Moyes aliyemrithi Sir Alex Ferguson kushindwa kufanya hivyo, mambo yamekuwa mchanganyiko Old Trafford.

Pamekuwapo vipindi vya ushindi lakini pia kupoteza mechi licha ya kuwa na kikosi kipana kilichosheheni nyota wa kimataifa.

Ni Januari hii Mourinho alifanya ingizo la mshambuliaji kutoka Arsenal, Alexis Sanchez, lakini hajapata matunda yaliyotarajiwa.

Kwa kifupi hazalishi kama alivyokuwa Arsenal huku mchezaji ghali zaidi klabuni hapo, Paul Pogba akiwekwa benchi mechi kadhaa baada ya kuelekea kutoelewana na Mourinho kwa sababu mbalimbali.

Habari zinasema kwamba bosi Mourinho amekuwa akiwakoromea wachezaji wake nyota kutokana na jinsi wamekuwa wakicheza, lakini pia wachezaji waandamizi wandaiwa kumlalamikia kocha huyo kwa mbinu na mfumo wake ambao unakwenda kinyume na namna wachezaji hao wanavyoweza kujipanga.

Kwa ujumla inaelezwa kwamba kuna mchezo wa kutupiana lawama hapo wakati United wakiachwa kwa mbali sana na Manchester City na wakiwa wameshakiri kwamba hawataupata ubingwa msimu huu.

Pia, anaelezwa kuwa amekabiliana na bodi ya wakurugenzi akiwalalamikia kwa kutopewa fedha za kutosha kama Pep Guardiola wa Man City na sasa anataka kufanya pangua pangua kiangazi cha mwaka huu.

Taarifa za ndani zinasema kwamba, hadi wachezaji tisa wanaweza kukabiliana na panga la Mourinho, wa waziwazi wakiwa ni pamoja na beki Luke Shaw, ambaye ni muda sasa wamekuwa wakikwaruzana hadharani. Pia, Daley Blind aliyeletwa na Van Gaal, ambaye amepata kuwa bosi wa Mourinho klabuni Barcelona. Mourinho anapata ahueni kwamba, kuna muda wa mapumziko kupisha michezo ya kimataifa kwa timu za taifa kwa sababu wachezaji wake walionekana kuchoka na kuelekea kupoteza mwelekeo.

Mourinho alitoa hotuba mfululizo kwa dakika 12 akiachia ‘povu’ baada ya mechi dhidi ya Brighton, akisema wachezaji walishindwa kuonesha haiba, kujituma na kukosa kiwango kinachotakiwa uwanjani.

Mourinho alifanya mkutano na Makamu Mtendaji Mkuu wa United, Ed Woodward ambaye ni mhusika mkuu wa usajili, na walikuwa pamoja Carrington Alhamisi wiki jana, Mourinho akitaka kuongeza wachezaji licha ya kuwa na kikosi cha pauni milioni 300.

Mourinho alisikika akilalamika kwamba, mambo yanapokuwa mabaya huachiwa peke yake, lakini wakishinda ni wote hujiona wamefanya vyema, akisema wanaposhinda wanashinda pamoja lakini wakipoteza mechi hubaki yeye mwenyewe na mzigo wa lawama bila usaidizi.

Mourinho anasema kuna wachezaji katika kikosi chake wanaogopa kucheza na kwamba, kuna waliokuwa wakimwambia waziwazi kuwa awaondoe uwanjani.

Wachezaji wengine wanaotarajiwa kuondoka ni Matteo Darmian, Marouane Fellaini, na pia labda Ander Herrera, Anthony Martial, Juan Mata na Chris Smalling huku nahodha Michael Carrick, ambaye anastaafu mwishoni mwa msimu huu.