Mourinho katika presha mpya

London, England. Kocha wa Manchester United, Jose Mouriho ameingia hofu ya kumpoteza libero wake Eric Bailly mwenye maumivu ya kifundo cha mguu.

Mourinho alidokeza Bailly anatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina kubaini ukubwa wa jeraha hilo ambalo linaweza kupunguza kasi ya Man United.

Man United inachuana vikali kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu dhidi ya mahasimu wake Manchester City inayoongoza kwa pointi 46.

Mourinho alisema kuwa endapo beki huyo wa kimataifa wa Ivory Coast hatapata matibabu ya kina, anaweza kupata matatizo makubwa siku za usoni.

Bailly aliyeumia wakati akiitumikia timu ya taifa ya Ivory Coast katika mashindano ya kimataifa, amekosa mechi nane za Man United kutokana na jeraha.

“Nadhani ana tatizo kubwa. Tunapambana ili apate matibabu ya kina, lakini tunaangalia kama anaweza kufanyiwa upasuaji baada ya kupata taarifa ya daktari,” alisema Mourinho.

Mourinho alisema hawezi kutabiri kama beki huyo anaweza kukosa mechi zote zilizobaki na ametoa nafasi kwa daktari kuendelea na uchunguzi.

Man United inaendelea kuwatumia mabeki wa kati Chris Smalling, Phil Jones au Victor Linderlof aliyesajiliwa na klabu hiyo majira ya kiangazi msimu uliopita.