Mourinho ampandia dau beki Spurs

Muktasari:

Spurs na  Man United zina historia ya kuuziana wachezaji akiwemo nahodha Michael Carrick na Dimitar Berbatov waliotua Old Trafford.

LONDON, ENGLAND. MANCHESTER United imepanga kumtoa beki wa kushoto Luke Shaw na Pauni 40 milioni kupata saini ya Danny Rose.

Man United inahaha kunasa saini ya beki huyo wa kushoto wa Tottenham Hotspurs na timu Taifa ya England.

Kocha wa Man United Jose Mourinho amekuwa na mapenzi ya muda mrefu kutaka kumsajili beki huyo mwenye kiwango bora.

Shaw amekosa namba kikosi cha kwanza na Mourinho amelazimika kumrusha kiungo wa pembeni Ashley Young kucheza beki wa kushoto.

Mouriho hakubaliani na uwezo wa beki huyo wa zamani wa Swansea tangu alipotwaa nafasi ya Louis Van Gaal baada ya kutimuliwa Chelsea.

Hata hivyo, Man United imekuwa katika mazingira magumu ya kumpata beki huyo baada ya kocha wa Spurs Mauricio Pochettino kuweka ngumu.

Spurs imekuwa ikimuwekea ngumu mchezaji huyo kuondoka makao makuu White Hart Lane kutokana na umuhimu wake katika kikosi cha kwanza.

Baada ya kubanwa muda mrefu na Man United, klabu hiyo ilimuweka sokoni beki huyo ikitaka Pauni50 milioni.

Rose mwenye miaka 27, amekuwa katika kipindi kigumu msimu baada ya kuandamwa na majeraha.

Shaw ameonyesha dhamira ya kuondoka Man United, baada ya kukwaruzana na Mourinho kwenye mazoezi kabla ya mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Brighton mwezi uliopita.

Spurs na  Man United zina historia ya kuuziana wachezaji akiwemo nahodha Michael Carrick na Dimitar Berbatov waliotua Old Trafford.