Mourinho amgeukia Willian

Muktasari:

Kiungo huyo Mbrazil amekuwa katika wakati mgumu ndani ya kikosi cha Chelsea

London, England. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, amemgeukia kiungo wa pembeni wa Chelsea, Willian.

Man United imeweka bayana kuwa inataka kumsajili winga huyo katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Willian amekuwa na kiwango bora katika kikosi cha Chelsea ingawa siyo chaguo la kwanza kwa kocha Mtaliano Antonio Conte.

Mourinho ameingia sokoni kutaka kiungo wa pembeni anayeshambulia kutoka kushoto ili kuimarisha kikosi chake katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Wiki iliyopita kocha huyo wa zamani wa Chelsea, alisema anafuatilia kwa karibu maendeleo ya Gareth Bale wa Real Madrid ambaye amekuwa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na majeraha ya kifua na misuli.

Mourinho alisema endapo mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales atakuwa fiti, atampa mkataba katika usajili wa majira ya kiangazi.

Mourinho anaweza kumsajili Wallian baada ya kuripotiwa kuwa hana furaha Makao Makuu Stamford Bridge.

 “Nataka kucheza mechi nyingi, lakini nakubali uamuzi wa kocha katika kupanfa kikosi,” alisema Willian.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye miaka 29, hakuwahi kuanza katika kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu England msimu.

Man United imemgeukia winga huyo baada ya kumsajili kiungo mkabaji Nemanja Matic kutoka Chelsea majira ya kiangazi msimu uliopita.