Mourinho: Lukaku kuliamsha kwa Leicester City

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo, aliyeiwakilisha Ubelgiji na kumaliza nafasi ya tatu katika fainali za Kombe la Dunia 2018, alirejea mazoezini mapema tofauti na wenzake licha ya kuwa na ruhusa ya kuendelea kupumzika.

London, England. Mshambuliaji mahiri wa Ubelgiji, Romelu Lukaku amemwambia Kocha wake Jose Mourinho, kuwa anataka kuanza katika mchezo wa leo kati ya Manchester United na Leicester City.

Mshambuliaji huyo, aliyeiwakilisha Ubelgiji na kumaliza nafasi ya tatu katika fainali za Kombe la Dunia 2018, alirejea mazoezini mapema tofauti na wenzake licha ya kuwa na ruhusa ya kuendelea kupumzika.

Mourinho, aliyeshangazwa na ujasiri huo, alisema kuwa anavyomuona Lukaku, ni mchezaji anayetaka kuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo, ingawa anadhani bado hajawa na nguvu za kutosha kuhimili mikikimikiki ya Ligi Kuu England, kwani alitumia nguvu nyingi katika fainali za Kombe la Dunia.

Kocha huyo alimjumuisha Lukaku katika mazoezi ya pamoja na wenzake mapema wiki hii kwenye uwanja wa Carrington, ikiwa ni ishara kuwa anaandaliwa kuongoza mashambulizi dhidi ya kikosi cha Kocha Claude Puel.

Wachezaji wa United walioziwakilisha nchi zao kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia ni Jesse LingardMarcus Rashford na Phil Jones walioiwakilisha England iliyofika nusu fainali wakati Ashley Young alicheza mchezo wa kutafuta nafasi ya tatu.

Naye Marouane Fellaini wa Ubelgiji na Paul Pogba wa Ufaransa walitumika katika mechi zote za hadi fainali, lakini waliomduwaza Mourinho, mbali ya Lukaku, ni Jones na Rashford waliokatisha mapumziko yake.