Morata kuibeba Chelsea Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

  • Chelsea imeshinda mechi zake mbili za awali kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo ushindi huo unakifanya kikosi cha Conte kuingia uwanjani kikiwa na ujasiri.

Mshambuliaji wa Chelsea, Alvaro Morata sasa ameanza mazoezi ya siku tatu kabla ya kikosi chake kushuka kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumatano.

Kikosi cha Chelsea kitashuka dimbani kuivaa Roma mchezo unaotajwa kuwa na ushindani mkali kutokana na rekodi ya klabu hizo kwenye mashindano hayo makubwa barani Ulaya.

Hata hivyo, Blues watamkosa Michy Batshuayi ambaye aliumia kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace ambayo Chelsea walipokea kipigo juzi Jumapili.

Kocha Antonio Conte ameonyesha furaha kutokana na kuwa na uhakika wa kurudi Morata kwenye mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Stamford Bridge.

Chelsea inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa imejiweka kwenye nafasi nzuri baada ya kushinda mechi zake mbili za awali dhidi ya Qarabag na Atletico Madrid.