Mo Rashid aanza kula mbivu Simba

Muktasari:

Mo aliyetua Msimbazi akitokea Prisons Mbeya, alisema kucheza na Emmanuel Okwi na John Bocco kumemfanya kupata mzuka, kwani ni wanaojitambua na kuiheshimu kazi yao.

NYOTA mpya wa Simba, Mohamed Rashid 'Mo' amekiri kuanza kula matunda ndani ya kikosi hicho, akitaja sababu kubwa ni kucheza na mastaa aliokuwa anatamani kufikia uwezo huo hasa alipoenda kambini ya Uturuki.
Mo aliyetua Msimbazi akitokea Prisons Mbeya, alisema kucheza na Emmanuel Okwi na John Bocco kumemfanya kupata mzuka, kwani ni wanaojitambua na kuiheshimu kazi yao.
"Naamini juhudi zangu ndizo zitakazofanya niendelee kuona matunda zaidi ya haya, nimegundua vitu vingi kwa Okwi na kujua kwa nini kila anapokuja kucheza  Tanzania, anakuwa na heshima kubwa dhidi ya nyota wenzake wa kigeni," alisema.
Mo alisema baada ya kutoka Uturuki ndoto zake zimeanza kukua na kutamani kufika mbali zaidi,  akidai ataelekeza nguvu kuhakikisha anapata namba ndani ya kikosi cha kwanza cha Kocha Patrick Aussems na msaidizi wake Masoud Djuma.
"Ingawa katika nafasi yangu kuna wachezaji wenye uzoefu na umakini wa juu kama Middie Kagere, Okwi na Bocco, hawatafanya niogope kupambania namba na uzuri ni watu wanaoshauri mtu anayejituma na kuonyesha anataka kwenda wapi."