Mna Ngoma sisi tuna Wawa

Muktasari:

  • Hata hivyo beki wa Simba, Mghana Asante Kwasi, akizungumza kabla ya kutimka Uturuki na kikosi cha Simba alisema ujio wa straika huyo Mzimbabwe hawauhofii kwa vile tayari kikosini kwao kuna watu wa kazi akiwamo Pascal Sergie Wawa.

BEKI kiraka wa Simba, Asante Kwasi wala hajashtushwa na usajili wa Donald Ngoma pale Azam akitokea Yanga. Ngoma aliyekuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi ametua Azam baada ya kusitishiwa mkataba na Yanga na mashabiki wanataka kuona atakuwa na jipya gani uwanjani.

Hata hivyo beki wa Simba, Mghana Asante Kwasi, akizungumza kabla ya kutimka Uturuki na kikosi cha Simba alisema ujio wa straika huyo Mzimbabwe hawauhofii kwa vile tayari kikosini kwao kuna watu wa kazi akiwamo Pascal Sergie Wawa.

Kwasi alisema anajua Azam imefanya usajili mkubwa akiwamo Ngoma na wengine, lakini wanaweza kukabiliana nao kwani Wawa si mchezo.

“Kweli kabisa Azam imesajili lakini hata sisi tupo vizuri kwani kikosi kilichocheza Kagame kimefanya vizuri, Wawa tumemuona akiongoza ulinzi vizuri nina imani mpaka ligi itakapoanza atakuwa vizuri zaidi, hata huyo Ngoma hatoweza kutusumbua,” alisema.

Akizungumzia ushindani katika msimu ujao, alisema kwamba hali itakuwa tofauti huku akikiri ongezeko la timu za VPL mpaka 20 ni changamoto mpya.