Mmemsikia Manji lakini

Muktasari:

Manji aliyekuwa akihojiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi kwa tuhuma ambazo hazijaelezwa, alipelekwa hospitalini hapo juzi jioni akiwa ndani ya gari la wagonjwa na baadaye gari lake kuonekana nje ya jengo hilo.

ULINZI mkali umeimarishwa kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikolazwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ambaye alikuwa akihojiwa na Polisi.

Manji aliyekuwa akihojiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi kwa tuhuma ambazo hazijaelezwa, alipelekwa hospitalini hapo juzi jioni akiwa ndani ya gari la wagonjwa na baadaye gari lake kuonekana nje ya jengo hilo.

Mwanaspoti ilifika katika taasisi hiyo na kushuhudia askari wenye sare na wengine wakiwa na mavazi ya kiraia wakiwa nje ya wodi aliyolazwa Manji ambaye pia ni diwani wa Mbagala.

Ilipofika saa 4:13 asubuhi mfanyabiashara huyo alitoka kwenye chumba hicho na kuongozwa kuelekea upande mwingine. Akiwa amevalia mavazi ya wagonjwa, Manji alitembea taratibu kuelekea upande aliokuwa akielekezwa.

Chanzo cha habari kililiambia Mwanaspoti kuwa mfanyabiashara huyo alipelekwa hospitalini baada ya kupoteza fahamu akiwa Polisi. Alisema licha ya madaktari kuendelea kumfanyia uchunguzi kujua chanzo cha tatizo hilo Manji ametaka kuruhusiwa akatibiwe nje ya nchi.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Profesa Mohamed Janabi alisema hawezi kuzungumzia taarifa za mgonjwa. Manji alikwenda kituoni hapo Alhamisi iliyopita na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Askofu Josephat Gwajima ambaye yeye aliachiwa Februari 11.

 

MAPOKEZI MAKUBWA WACHEZAJI

Baada ya ushindi mnono ugenini juzi kwenye mechi ya kwanza ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Yanga umewaandalia mapokezi makubwa wachezaji wao ambao watawasilia saa tano asubuhi ya leo Jumanne jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Ni kweli tumeandaa mapokezi makubwa kwa timu yetu ambayo tunatarajia itawasilia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kati ya saa 4:30 hadi saa 5 asubuhi ambapo watalakiwa uwanjani na mashabiki wao.”

Akizungumzia maandalizi ya mchezo wao na Simba utakaofanyika Februari 25, Mkwasa alisema baada ya timu kuwasili wataweka mikakati na benchi la ufundi kuelekea kwenye mchezo huo.

“Tumemaliza hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na sasa tunaelekeza nguvu kwenye ligi, lengo la kila Mwanayanga ni ushindi hivyo nguvu, akili na malengo yetu tunayarudisha kwenye ligi katika mchezo ujao,” alisema.

Mkwasa ambaye kitaaluma ni kocha wa soka mwenye leseni ya kimataifa alisema kambi ya kuelekea kwenye mchezo huo wa watani wa jadi itapangwa na benchi la ufundi mara baada ya timu kuwasili asubuhi.

Yanga imeanza kwa kishindo mashindano ya Klabu Bingwa Afrika ikiwa ugenini baada ya kuicharaza Ngaya ya Comoro mabao 5-1 juzi Jumapili na baada ya mechi rahisi ya marudiano jijini Dar es Salaam, Yanga itacheza na mshindi kati ya Zanaco na APR ya Rwanda. Zanaco tayari imelazimishwa suluhu nyumbani.