Mmeisikia kauli ya Kichuya lakini?

WINGA wa Simba, Shiza Kichuya, amesema kitendo cha timu yao kuvuna pointi sita na mabao mawili mkoani Mbeya, kimeacha historia mpya inayoonyesha ubora wao.

Kichuya ndiye aliyefunga bao katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City huku John Bocco akifanya hivyo kwenye ushindi kama huo dhidi ya Prisons.

“Hakuna kitu kibaya kama akili kujijenga kuwa mnapoenda sehemu fulani mtakwama, hivyo kuwafunga Prisons na City, kumetuongezea kujiamini kama tukiweka dhamira ya dhati kwa kila mechi inawezekana,” alisema.

“Haikuwa kazi rahisi kuzifunga Prisons na City, kwani ni timu zenye uwezo wa juu, kikubwa tunashukuru kuondoka mkoa huo kwa kutembea kifua mbele na kurejea Dar es Salaam na pointi sita,” alisema.

Naye Ally Shomary alisema ushindi huo umeonyesha ukongwe wa klabu hiyo, akidai ushindani ulikuwa wa hali ya juu uliotokana na mwamko wa wakazi wa Jiji hilo walivyofika kuziunga mkono timu zao.

“Unajua mashabiki ni sehemu ya kunogesha mchezo, hao wakazi wa jiji hilo wana amsha amsha kama ulivyo mkoa wa Shinyanga, kutokana na hilo lazima wachezaji wakae sawa na kujua vita si rahisi, tunashukuru tumefanikiwa,” alisema.

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni, alisema ushindi huo ni hatua kubwa kwani umewahakikishia kukaa kileleni huku wakiendelea kujipanga na mechi zilizopo mbele yao.

“Kushinda mechi zote mbili si kazi ndogo, nawapongeza wachezaji kwa umakini waliouonyesha, wasijisahau bado safari ni ndefu, wajipange ili waendelee kukaa kileleni,”alisema.