Mkongo wa Yanga hakisomeki

Muktasari:

  • Awali iliripotiwa kwamba mchezaji huyo anayecheza nafasi ya beki wa kati, atatua kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi akisaidiana na Andrew Vincent ‘Dante’ pamoja na Kelvin Yondani baada ya uongozi kupokea maelekezo kutoka kwa Kocha Mkuu Mwinyi Zahera.

UNAMKUMBUKA yule beki Fally Mlumba, ambaye ilikuwa inadaiwa kwamba atatua kujiunga na klabu ya Yanga muda wowote, basi ukimya umezidi kutanda kwa mchezaji huyo.
Awali iliripotiwa kwamba mchezaji huyo anayecheza nafasi ya beki wa kati, atatua kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi akisaidiana na Andrew Vincent ‘Dante’ pamoja na Kelvin Yondani baada ya uongozi kupokea maelekezo kutoka kwa Kocha Mkuu Mwinyi Zahera.
Mwanaspoti lilimtafuta na kufanya naye mazungumzo, ili kufahamu kinachoendelea baina yake na Yanga ambapo alifunguka kwamba walielewana kila kitu lakini walimwambia watarudi kwake kitu ambacho kimekuwa tofauti.
“Ni kweli nilizungumza nao muda mrefu na kuelewana nao baadhi ya vitu, niliwaambia waende wakaonane na Uongozi wangu, waliniambia kwamba watarudi tena kwangu lakini tangu hapo wapo kimya,” alisema.
Fally aliongeza kwamba mkataba wake na Bandari bado upo na hiyo ndio sababu kubwa ya yeye kuwataka kwanza wamalizana na Uongozi ili ajue anafanyaje baada ya kupata majibu.
"Nilitaka kwanza nisikie majibu yao baada ya kuzungumza na viongozi, lakini hawajaniambia kilichoendelea sasa ni ukimya,pia mimi naweza nikaamua kuhusu mkataba wangu kama nikipata jibu na sio sasa hivi,” alisema.
Mkongo mwingine ambaye Yanga wamemkaushia ingawa walikuwa wanamuhitaji kutoka Bandari ni Yema Mwana anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alikuwa anatajwa kuja kucheza nafasi ya Donald Ngoma ambaye amejiunga na Azam FC.