Mkongo wa Alliance amtumia salamu Okwi

Muktasari:

Mshambuliaji huyo Mkongo Chinedu ameanza kuthibisha ubora wake baada ya kufunga bao wakati Alliance ikichapa  Kagera Sugar kwa mabao 2-1 katika mchezo wa  kirafiki huku bao lingine likifungwa na Mnyarwanda Weyeka Tatue.

Mwanza. Mshambuliaji mpya wa Alliance FC, Chinedu Michael amemtaka mfungaji bora wa msimu uliopita Emmanuel Okwi wa Simba kujiandaa kisaikolojia katika vita ya kuwania tuzo ya ufungaji bora msimu huu.
Mshambuliaji huyo Mkongo Chinedu ameanza kuthibisha ubora wake baada ya kufunga bao wakati Alliance ikichapa  Kagera Sugar kwa mabao 2-1 katika mchezo wa  kirafiki huku bao lingine likifungwa na Mnyarwanda Weyeka Tatue.
Chinedu alisema malengo yake katika Ligi Kuu ya Tanzania ni kufanya vizuri na kuibuka mfungaji bora na kuwa amejiandaa vyema kukabiliana na ushindani wa aina yoyote.
Alisema kuwa majukumu ya mshambuliaji yeyote ni kufunga mabao hivyo anaamini kwa ushirikiano na wenzake, nidhamu na kujituma kwake ndivyo vitamfikisha katika malengo aliyoweka.
Aliongeza kuwa mbali na kupambana kusaka kiatu cha dhahabu, atahakikisha anaisaidia timu yake kufanya vizuri na kuonyesha ushindani katika michuano hiyo mikubwa hapa nchini.
“Hii ndio mara yangu ya kwanza kucheza hapa nchini, sijui makali yoyote ya mchezaji kwa hiyo nitaipambania timu bila kujali tunakutana na nani,hii ndio kazi yangu hivyo niombe ushirikiano,”alisema Mkongo huyo.