Yanga yafunga usajili kimtindo

Muktasari:

  • Dirisha dogo la usajili wa Tanzania Bara limefungwa saa 6 usiku Ijumaa

 Kabla ya Waislam hawajaingia katika swala Ijumaa tayari Yanga ilishathibitisha kwamba hakuna usajili mpya wowote utakaofanywa.

Aliyetoa kauli hiyo ya tamati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika aliiambia tovuti ya www.Mwanaspoti.co.tz  kuwa usajili wao katika dirisha dogo umefungwa kwa kuwaingiza wachezaji wawili pekee.

Nyika ameshalamba shavu la kuongoza kamati ya Mashindano akisaidiana na makamu wake Mustapha Ulungo amesema hatua ya kumalizana na beki Mkongomani Fistoo Kayembe na mshambuliaji kinda Yohana Mkomola ndiyo kilikuwa kikomo cha usajili huo.

Bosi huyo alisema walitaka kufanya usajili wa maana katika kuboresha safu yao ya ushambuliaji lakini muda mfupi wa usajili ulikwamisha zoezi kwa kupatikana vifaa vya maana ambavyo walipanga kuvitafuta.

"Huku Yanga msihangaike sana kuangalia tutafunga vipi usajili, tumeshamaliza hilo jukumu kwa kuingiza hao wachezaji wawili tu hatutasajili tena mpaka wakati mwingine,"alisema Nyika.

"Tulipanga kufanya usajili mkubwa lakini muda umekuwa mfupi lakibni pia kama mnavyojua usajili sio kitu cha kukurupuka tulisema tunatafuta kiungo tukamleta Pappy (Tshishimbi) watu wakaridhika,tulisema tunataka mshambuliaji tukamshusha Ajib (Ibrahim) hakuna asiyeridhika kwahiyo tulitaka kufanya kweli, lakini tukakosa kile tunachotaka.

"Kama uongozi tunataka kufanya uamuzi makini ili yawe na tija kwa klabu na kocha wetu alituambia kama tunasajili mchezaji basi awe mzuri kuliko yule anayetoka na hapo ndipo tunapiopasimamia kama viongozi."