Mkomola huyo atimkia Etoile Du Sahel

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Serengeti  Boys, Yohana Mkomola ametimkia nchini Tunisia kwenda kujiunga na Etoile Du Sahel, akiwa na wenzake wawili, Enrick Vitalis Nkosi  na Hamis Ng'anzi waliokwenda kufanya  majaribio.

Mkomola alifanya majaribio mwanzoni mwa  mwaka huu na kufaulu, atajiunga moja kwa moja na kuanza kucheza wakati Nkosi na Ng'anzi  watafanyiwa majaribio kwa kipindi cha siku 15.

Mshambuliaji huyo aliyepata umaarufu ndani ya Serengeti hasa katika mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana nchini Gabon ameondoka  na ndege ya shirika la ndege la Uturuki.

Alisema: "Namshukuru Mungu kupata nafasi hii, kwangu ni tukio muhimu na nafikiri kila mmoja anatambua hilo, ninachoweza kusema, naenda kupanda, kufanya kazi kwa nguvu kuhakikisha nafanikiwa, kikubwa Watanzania wenzangu waniombee."

Meneja wa wachezaji hao kutoka kituo cha Cambiaso na kaka wa Mkomola, Stanley Mkomola alisema, anafurahi kuona wachezaji hao wanapata nafasi kama hizo, akasisitiza Watanzania wawaombee.