Mkomola aenda Etoile na wengine wa Serengeti Boys

MSHAMBULIAJI tegemeo wa Serengeti Boys, Yohana Mkomola, amepaa kwenda Tunisia kuanza kuitumikia klabu ya Etoile du Sahel ya huko akiongozana na Erick Vitalis Nkosi na Hamis Ng’anzi wanaokwenda kwa ajili ya majaribio.

Mkomola anakwenda kujiunga na klabu hiyo iliyowahi pia kumsajili mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi. Straika huyo wa timu hiyo ya vijana ya taifa, amepata dili hilo baada ya kufanya majaribio mwanzoni mwaka huu na wakiwa katika  mazungumzo ya mkataba, aliitwa kuja kuichezea Serengeti katika mashindano ya Afrika kule Gabon.

Hapo Etoile ataanza kukitumikia kikosi cha vijana wa umri chini ya miaka 20 kwa makubaliano maalumu yaliyofanywa baina ya kituo chake cha Cambiaso na klabu hiyo.

Meneja wa mchezaji huyo ambaye pia ni kaka yake, Stephano Mkomola amesema itakapopofika Februari mwakani, atakuwa amefikisha miaka 18 na hapo ndio atakapokaa nao tena na kusaini mkataba rasmi.

“Tunashukuru dogo amefanikiwa, ni faida ya kila Mtanzania kikubwa tumwombee kwa anachokwenda kufanya afanikiwe,” alisema kaka huyo kuhusu mdogo wake aliyeondoka jana Alhamisi asubuhi.

Kuhusu hao wengine, alisema wamepata mwaliko wa kufanya majaribio kwa siku 15.

“Muda mfupi kabla ya kupanda ndege, Mkomola alisema: “Kikubwa mniombee tu, naenda nikiwa mwenyeji kwa sababu mazingira yake nilishaanza kuyazoea wakati wa majaribio. Nitajitahidi,” alisema.