Mke wa King Majuto hajaonekana arobaini ya mumewe

Muktasari:

Wakati wa uhai wake King Majuto ameigiza katika filamu nyingi na wasanii tofauti akiwemo, Jacob Steven 'JB'.

Tanga. Mke wa King Majuto anayeitwa, Aisha Yusuph ameshindwa kufika katika kisomo cha arobaini ya mume wake iliyosomwa nyumbani kwa msanii huyo Donge jijini Tanga na kitendo hicho, kimeishangaza familia ya msanii huyo na sehemu ya wageni.

Majuto ambaye alikuwa maarufu nchini na Afrika Mashariki  kutokana na kazi yake ya kuchekesha, alifariki mwezi Agosti mwanzoni baada ya kuugua kwa kipindi kirefu ugonjwa wa Tezi Dume.

Ambapo, alitibiwa nchini, akafanyiwa upasuaji sambamba na kupelekwa India kwa ajili ya matibabu zaidi lakini aliporudi, siku chache baadaye alifariki.

Wakizungumza nyumbani kwa msanii huyo Donge jijini Tanga mjomba  wa King Majuto anayeitwa, Hamza Kasongo pamoja na watoto wa marehemu ambao ni Mohammed na Hamza Amri walisema, wao hawana kinyongo na mama huyo na hawajamfukuza.

Kasongo ambaye pia ni mwalimu wa sanaa wa King Majuto alisema, kitendo cha mke wa King Majuto kutohudhuria katika shughuli hiyo kinaonyesha ana kinyongo na familia wakati bado inampenda na haijamtenga.

"Kitendo cha kutohudhuria arobaini siku ya leo, kufunga na makufuli nyumbani Dar es salaam na kuhamisha vyombo, kinaleta picha mbaya kwa jamii ionekane ananyanyaswa wakati si kweli," alisema Kasongo.

Mjomba wake huyo ambaye pia ni msemaji wa familia ya king Majuto amesema mara baada ya shughuli hiyo ya arobaini watakaa kwa ajili ya kuweka sawa mambo yote.

Mohamed Majuto amesema, licha ya watoto wa marehemu King Majuto walizaliwa kwa mama tofauti lakini wanamtambua Aisha ni mama yao na hawako tayari kuona dosari baina yao.

"Huyu ni mama yetu tunamthamini na kumtambua kwa hivyo hatuko tayari kuona akihangaika baada ya baba yetu kufariki,"alisema Hamza.

Hamza ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo alisema familia ya King Majuto imelelewa kidini na hata kabla ya kufariki baba yao aliwaambia wapendane.

MKE WA MAJUTO AZUNGUMZA

Kwa upande wa Aisha alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi, alisema, hajawa tayari kuzungumza na vyombo vya habari.

"Sipo tayari kuzungumza na vyombo vya habari leo (Septemba 15) naomba nipumzike," alijibu Aisha.

Shughuli hiyo ya arobaini ilihudhuriwa na watu kutoka mikoa mbalimbali nchini kama waaandishi na wasanii .