Mil 800 Yanga zaitega Simba

Muktasari:

  • Mabosi hao wa Yanga waliamua kuitana ghafla na kukaa faragha katika moja ya hoteli kali jijini Dar es Salaam na kupanga mipango yao ya usajili na ndipo ikawekwa mezani bajeti kwamba ili kila kitu kikae sawa zinahitajika Sh800 milioni.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, anatarajia kutua nchini leo Ijumaa akitokea Ufaransa kwenye mapumziko, lakini huku nyuma mabosi wake kupitia kamati za vigogo wamefanya jambo moja la maana na iwapo litatiki lazima Simba iisome namba.

Mabosi hao wa Yanga waliamua kuitana ghafla na kukaa faragha katika moja ya hoteli kali jijini Dar es Salaam na kupanga mipango yao ya usajili na ndipo ikawekwa mezani bajeti kwamba ili kila kitu kikae sawa zinahitajika Sh800 milioni.

Fedha hizo zinaelezwa zinaweza kuwatikisa na kuwapeleka puta watani wao Simba ambao kwa sasa wanatambia uwepo wa Bilionea Mohammed ‘MO’ Dewji.

Yanga kwa sasa inapiga hesabu itoke vipi katika kuingia kwenye dirisha la usajili utakaoweza kurudisha heshima ya klabu yao ambayo imeyumba mpaka kunyoosha mikono wakitaka tajiri wao Yusuf Manji arejee haraka klabuni.

Kinachowaumiza kichwa Yanga ni nguvu ya fedha za MO Dewji ambaye mpaka sasa hajapata mpinzani labda Manji arudi, ndipo ikabainishwa kiasi hicho kisichopungua Sh800 milioni kinaweza kumtikisa MO na Simba yake.

Habari zilizonaswa na Mwanaspoti kutoka ndani ya Yanga ni kama bajeti yao kamili itaweza kukidhi mahitaji ya kukamilisha kuundwa kwa kikosi cha maana ambacho wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanahitaji kukiona.

Taarifa zaidi zinasema kuwa Kamati Maalum chini ya Mwenyekiti Abbas Tarimba wiki hii ilifanya kikao chake cha kwanza na kukubaliana mambo kadhaa muhimu ambayo hajayawekwa wazi kutokana na kuamua kufanya mambo yao kimya kimya.

Inaelezwa fedha hizo zinahitajika ili kumudu majukumu yao, ikiwamo kumalizana na wachezaji waliomaliza mikataba yao sasa.

Ndani ya jukumu hilo Yanga inatakiwa kwanza imalize kulipa malimbikizo ya ada za usajili katika mikataba ya wachezaji wao waliotumika misimu miwili iliyopita ambazo zilikuwa hazijamaliza na uchunguzi kuonyesha si chini ya Sh120 milioni zinahitajika hapo.

Wakitoka hapo kazi itakayofuata ni kulipa mishahara ya timu nzima kwa miezi mitatu ambapo kwa mwezi mmoja si chini ya Sh140 milioni zinahitajika kwa hesabu hizo kumudu kulipa miezi yote mitatu kiasi cha Sh420 milioni kinahitajika haraka.

Majukumu hayo mawili yakimalizwa sasa, ndipo litaanza jukumu la kufikiria usajili mpya ambapo pia kamati ya Tarimba yenye jukumu la kusaka fedha ikishirikiana na Kamati ya Usajili chini ya Mwenyekiti, Hussein Nyika na kazi hiyo itaanzia kwa wanaotakiwa kubakizwa kwa kuongezewa mikataba.

Kundi hilo la wachezaji litaongozwa na Nahodha Msaidizi, Kelvin Yondani, Andrew Vincent ‘Dante’, Juma Abdul, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, kipa Benno Kakolanya, Juma Mahadhi ambao Mwanaspoti linafahamu benchi la ufundi limetaka wabakizwe.

Baada ya hapo Yanga itatinga kuanza kusajili wachezaji wapya katika kuongeza nguvu katika kikosi chao wakihitajika mastraika wawili, kiungo mmoja na beki wa kati mmoja wote hao wa kigeni huku beki wa kulia au kushoto naye akihitajika.

SIMBA YANGA ZAIBEBA

Simba imetamka kwamba usajili wao kwa wachezaji wa ndani umemalizika na sasa macho yao ipo kimataifa zaidi lakini pia akili kama hiyo ipo Azam ambayo imegoma kuanza kufikiria kuchukua wachezaji kutoka Simba na Yanga.

Mipango hiyo ya Simba na Azam ni kama wameamua kuifichia aibu Yanga kwa kuwachunia wachezaji wake muhimu ambao kama wangekunja uso basi kazi ingemalizika kirahisi.

Presha hiyo itaifanya Yanga kuwa na akili rahisi kumalizana na wachezaji wake hao ambao wanamaliza mikataba kutokana na kutokuwa katika vita ya kuwaniwa na timu nyingine kubwa hapa nchini.

MSIKIE TARIMBA

Mwanaspoti jana lilimtafuta Tarimba ambaye hata hivyo alisema kwa sasa wako katika majukumu mazito na kwamba masuala yote ya kazi zinazofanywa na kamati yake yatazungumziwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa baada ya kubaini kuna upotoshwaji mkubwa wa taarifa (sio kutoka magazeti ya kampuni ya Mwananchi) zisizo rasmi ambazo zimekuwa zikiharibu utulivu klabuni kwao.

“Kuhusu kuzungumzia tunachofanya sasa naomba mtafute Mkwasa ndiye tuliyemteua kuongelea kamati, kuna mambo yameripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo sijaongea navyo na kuleta usumbufu mkubwa kwangu na kwa klabu yetu kwa ujumla,” alisema Tarimba.