Mgunda, Alikiba wana siri yao

Muktasari:

Juzi baada ya gemu yao na African Lyon kumalizika kwa suluhu, huku Kiba akiwa jukwaani, ilifanya wanahabari kumbana Mgunda, lakini kocha huyo aliishia kujibu; “Nimesajili wachezaji 30 Kiba ni kati ya hao, atacheza tu mechi zinazoendelea.”

KUMEKUWA na maswali mengi juu ya usajili wa Alikiba ndani ya Coastal Union, huku mwimbaji huyo akishindwa kushuka uwanjani kucheza na hata Kocha wake, Juma Mgunda anapoulizwa amekuwa akijiumauma tu kuonyesha kuna siri nzito.

Juzi baada ya gemu yao na African Lyon kumalizika kwa suluhu, huku Kiba akiwa jukwaani, ilifanya wanahabari kumbana Mgunda, lakini kocha huyo aliishia kujibu; “Nimesajili wachezaji 30 Kiba ni kati ya hao, atacheza tu mechi zinazoendelea.”

Alipoulizwa hawaoni kama nafasi ya mwimbaji huyo inapoteza bure kwa vile jamaa anatingwa na ratiba yake ya kisanii na Kocha Mgunda alijibu; “Atajiunga tu kwani shida iko wapi, nimesema atacheza kwani ni mchezaji peke yake mbona hata waliocheza wamefanya vizuri tu ni mchezaji wangu atatumika tu kwa michezo ijayo.”

Katika mchezo huo wakati wachezaji wanaingia tayari kuanza mchezo, Alikiba aliongozana na Mgunda na baadhi ya viongozi akaenda mpaka sehemu ya wachezaji wa akina na kupiga stori mbili tatu kisha kuelekea jukwaani kukaa. Kitendo cha kukaa jukwani na wakati wapo baadhi ya mashabiki walitamani wamuone anacheza ndipo maneno yalianza kuhoji nafasi yake.