Mgomo Gor kumbe tatizo noti

Muktasari:

  • Nyota wa Gor waligomea kupokea medali za ushindi wa tatu wa michuano ya Kombe la Kagame sambamba na kugomea kuingia vyumba vya kubadilishia nguo kwa madai ya imani za kishirikina na kuadhibiwa na CECAFA Jumamosi.

SIKU moja baada ya kufungiwa miaka miwili na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), uongozi wa Gor Mahia ya Kenya umesema utawachukulia hatua nyota wake walioitia aibu ugenini klabu yao.

Nyota wa Gor waligomea kupokea medali za ushindi wa tatu wa michuano ya Kombe la Kagame sambamba na kugomea kuingia vyumba vya kubadilishia nguo kwa madai ya imani za kishirikina na kuadhibiwa na CECAFA Jumamosi.

Kitendo hicho kimewakera mabosi waMabingwa hao wa Kenya na SportPesa Super Cup, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, Ludovick Aduda aliliambia Mwanaspoti kitendo hicho ni cha aibu kwao kwani wachezaji na benchi la ufundi hawakupaswa kugomea medali hizo na kufichua chanzo cha yote hayo.

“Unajua mtindo wa kawaida ni kwamba zile pesa timu hupewa taslimu mkononi ila raundi hii sheria za nchi hairuhusu kiwango kikubwa kama hicho kupewa mkononi hivyo kuingizwakwenye akaunti ya klabu na wachezaji kukasirika,” alisema.

“Klabu itawachukulia hatua za kinidhamu wale wote walio waongoza wenzao kutenda Jambo la aibu kama hili,” alisema Aduda.

Alisema wao kama viongozi walikaa jukwaa kuu hivyo kushindwa kufanya lolote ili kuwalazimisha wachezaji kwenda kupokea medali kwani mpaka wanashuka kwenda chumbani tayari kitendo kilikuwa kimepita.

“Ni jukumu la kocha na meneja wa timu kwani ndio wako na wachezaji kiwanjani, kitendo cha sisi kuteremke kutoka VIP muda ilishapita,” alisema Aduda.

“Kesho (leo Jumatatu) tutakuwa na kikao cha viongozi ila tutamuita kocha ajieleze kwanini ilitokea vile na baadaye wachezaji wote wataitwa kuhojiwa, wametutia aibu na kutuingiza kwenye tatizo lisilotarajiwa.”

Kuhusu kugomea kuingia chumba cha kubaidlishia nguo, Aduda alisema litajadiliwa katika kikao hicho na atakuwa katika nafasi nzuri ya kulitolea ufafanuzi baada ya kikao chao hicho.