Mfaransa wa Lyon apania kuifunga Coastal Union

Muktasari:

African Lyon na Coastal Union zinakutana kwa mara ya kwanza tangu zilipopanda Ligi Kuu Bara msimu huu

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa African Lyon, Mfaransa Victor da Costa amesema maandalizi waliyoyafanya watapata ushindi wao wa kwanza dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

African Lyon imecheza mechi tatu na kuambulia pointi mbili kwa kutoka sare kwenye michezo miwili na kupoteza mmoja, itakuwa na kibarua kigumu kesho kwa kuikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

“Yanga walitupa kipimo cha maandalizi yetu kuelekea mchezo huu, naamini tupo tayari na tutaanza kuwashangaza wengi. Najua Lyon siyo timu kubwa hapa nchini, lakini inawachezaji wenye uwezo wa kupambana na kupata matokeo ya ushindi,” alisema mshambuliaji huyo.

Akizungumzia idadi ya mabao ambayo amejiwekea kufunga kwenye msimu wake wa kwanza, da Costa alisema ni mabao 10 licha ya changamoto ya ubovu wa viwanja vya mikoani.

Nyota huyo wa African Lyon alisema wenzake wamekuwa wakimweleza kuwa viwanja vya mikoani ni vibovu, lakini pamoja na ubovu wake atajitahidi kufanya kila litakalokuwa linawezekana ili afikishe idadi hiyo ya mabao.

Mbali na mchezo wa African Lyon dhidi ya Coastal Union, Mwadui ya Shinyanga itakuwa nyumbani kesho kwenye uwanja wao wa Kambarage mkoani Shinyanga kucheza dhidi ya Azam.