Messi kwa mataji haijapata tokea Barca

Barcelona, Hispania. Wakati Frank Rijkaard alipoamua kumchezesha Lionel Messi katika mechi ya LaLiga mwaka 2005, wachache walifikiri kuwa Muargentina huyo angeweza kutamba, lakini leo 2018 amekuwa ni mchezaji aliyetwaa mataji mengi zaidi kuliko mchezaji yeyote ndani ya Barcelona.

Ushindi wa Barcelona wa mabao 2-1 dhidi ya Sevilla nchini Morocco inamfanya Messi kufikisha rekodi ya kutwaa mataji 33, akiwa na miamba hiyo ya Catalan, akiwapiku Andres Iniesta na Gerard Pique.

Pep Guardiola alipoingia Camp Nou alikuwa na mafanikio makubwa zaidi japokuwa Messi ameendeleza rekodi hiyo ya bosi wake wa zamani.

Akiwa na kitambaa cha unahodha mkononi Messi amefanikiwa kunyakuwa taji la Supercopa de Espana.

Kabla ya mchezo huo wa jana, Iniesta na Messi walikuwa sawa kwa kuchukua mataji 32, lakini Mhispania huyo ametimkia Vissel Kobeit na kuacha mwanya kwa mwenzake kuweka rekodi mpya.

Wanaofuatia kwa karibu kwa kunyakuwa mataji mengi ni Sergio Busquets na Pique, wote wametwaa mataji 28, hata hivyo kutokana na umri wao ni wazi kuwa hawana nafasi ya kumpiku Messi.