Messi alivyoingia anga za wababe wa dunia

Muktasari:

  • Kwenye orodha hiyo ni mchezaji mmoja pekee ambaye anaendelea kugusa mpira huku wengine wote wakiwa tayari wameshastaafu. Wakali wenyewe hawa hapa.

KATIKA vitabu vya kumbukumbu za soka, ni wachezaji wanane tu walioweka rekodi ya kuifungia klabu moja zaidi ya mabao 500.

Kwenye orodha hiyo ni mchezaji mmoja pekee ambaye anaendelea kugusa mpira huku wengine wote wakiwa tayari wameshastaafu. Wakali wenyewe hawa hapa.

PELE

Klabu: Santos

Mabao: 619

Kulingana na shirikisho la kimataifa linaloshughulikia historia ya soka na takwimu zake IFFHS, Pele ndiye mfungaji bora wa nyakati zote duniani akiwa na rekodi ya jumla ya mabao 1281 aliyofunga katika mechi 1363 alizocheza kabla ya kustaafu.

Katika mabao hayo, 619 alifunga akiwa na kikosi cha Santos alichocheza kati ya 1956 na 1974. Mbrazili huyo alifunga idadi hiyo ya mabao katika mechi 638. Bado rekodi hiyo ya mabao 600 haijavunjwa.

GERD MULLER

Klabu: Bayern Munich

Mabao: 566

Muller anakumbukwa kuwa straika hatari akitajwa kuwa mmoja kati ya wamaliziaji wazuri kuwahi kushuhudiwa katika soka. Takwimu zinaonyesha kwa kipindi cha miaka 15 aliyochezea Bayern Munich, alicheza mechi 453 kati ya mwaka 1964 na 1979 na kufunga jumla ya mabao 566.

LIONEL MESSI

Klabu: Barcelona

Mabao: 546

Hadi kufikia wikendi hii, Messi alifikisha idadi ya mechi 632 alichozocheza kwenye kikosi cha Barcelona. Kabla ya kuzalilishwa na AS Roma kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wikiendi ile, Barca ilicheza na Leganes na Messi alifunga ‘hat-trick’ katika mechi hiyo. Mabao hayo yalimfanya Messi kufikisha 546 na hivyo anahitaji mabao 63 tu kufikia rekodi ya Pele.

FERNANDO PEYROTEO

Klabu: Sporting Lisbon

Mabao: 544

Alifariki dunia mwaka mmoja kabla ya Pele kustaafu. Kabla ya kifo chake akiwa na miaka 60, Fernando alikuwa straika hatari na maisha yake yote aliichezea Sporting Lisbon na alipachikia mabao 544 na kushinda mataji 11 ya ubingwa wa Ligi Kuu Ureno.

JOSEF BICAN

Klabu: Slavia Prague

Mabao: 534

Bican aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88, aliichezea Slavia zaidi ya mara 217 na ni katika mechi hizo aliweza kuifungia mabao 534. Bican anakumbukwa kwa kasi yake na uwezo wa kutumia miguu yote miwili kucheza mpira bila tatizo. IFFHS ilimtunuku kwa heshima ya kumpa tuzo ya Mpira wa Dhahabu huku ikimtaja kuwa ni mfungaji bora wa karne iliyopita.

JIMMY McGORY

Klabu: Celtic

Mabao: 522

Jimmy alifariki Oktoba 1982 akiwa na umri wa miaka 78. Alicheza soka lake wakati wa kipindi cha vita vya kwanza duniani kisha kuwa kocha katika kipindi cha vita vya pili duniani. Takwimu zilizopo zinaonyesha alishiriki jumla ya mechi 378 alipoichezea Celtic na ni katika mechi hizo ndipo aliweza kuingia kwenye kumbukumbu hii ya kuifungia timu moja zaidi ya mabao 500.

JIMMY JONES

Klabu: Glenavon

Mabao: 517

Naye alifariki dunia miaka minne iliyopita akiwa na miaka 85. Jimmy alijiunga na klabu iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu Ireland, Glenavon akitokea Fulham na katika kipindi hicho aliishia kuwa mfungaji bora kwenye ligi hiyo kwa miaka kadhaa. Hadi sasa rekodi zinaonyesha ndiye mfungaji bora wa nyakati zote katika Ligi ya Ireland. Huko Glenavon aliichezea mechi 222.

UWE SEELER

Klabu: Hamburg

Mabao: 507

Ujerumani inamtambua kuwa miongoni mwa mastraika wake hatari kuwahi kutokea. Seeler alicheza katika miaka ya 50 akitumia muda wake mwingi katika klabu ya Hamburger ambayo aliichezea jumla ya mechi 476 na kufunga mabao 507. Anakumbukwa kwa kuwa na mguu mkali wa kushoto ambao ulichongewa sanamu baada kustaafu soka.