Mechi kali tano, Simba na Ndanda ndani!

Muktasari:

Simba inacheza na Ndanda FC ukiwa ni mchezo wao wa tatu baada ya kuzifunga Tanzania Prisons na Mbeya City.

Dar es Salaam. Jumla ya viwanja vitano kuanzia mchana wa leo Jumamosi vitawaka moto wakati mechi za Ligi Kuu Bara zitakapokuwa zinachezwa.

Lakini, macho na masikio ya Watanzania wote yatakuwa kwenye mchezo wa saa 10:00 jioni wakati, Wekundu wa Msimbazi Simba watakapokipiga na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Mchezo huu unatarajiwa kuwa na watazamani wengi si mashabiki wa Simba tu, bali hata wale watani wao wa jadi Yanga, watataka kujua jamaa hao wanapata matokeo gani.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems pamoja na wachezaji wake wametamka hawana wasiwasi na mchezo huo ni ushindi tu.

Aussems amefurahishwa na uwepo wa wachezaji wake kama Mzambia cletus Chama na Emmanuel Okwi raia wa Uganda ambao mchezo huo utakuwa wa kwanza kwanza.

Katika Uwanja wa Samora mkoani Iringa utapigwa mchezo kati ya Lipuli FC dhidi ya Mtibwa Sugar saa 8:00 mchana, Uhuru utacheza mchezo kati ya KMC na Singida United saa 10:00 jioni.

Mechi nyingine itakuwa kati ya Mbao FC na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa CCM Kirumba saa 10:00 jioni na Tanzania Prisons watakipiga na Ruvu Shooting muda huo Uwanja wa Sokoine.