Mchongo wa Yanga ukitiki tu, mmeumia

Thursday October 12 2017Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga     

Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga      

By GIFT MACHA

WAKATI Simba ikiwa kwenye mchakato wa kumpata mwekezaji wa kumpa klabu yao kuingia kwenye mfumo mpya wa uendeshaji, viongozi wa Yanga wamekaa chini na kukuna kichwa ili kula sahani moja na watani zao.

Baada ya kujadiliana kwa kina, sasa wamekuja na mpango kabambe na kama mchongo huo utatiki basi, wanachama na mashabiki hiyo watakuwa wakitabasamu tu kwa furaha mitaani.

Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga amefichua kuna mambo wanayaweka sawa na kama yataenda alivyopanga basi klabu hiyo itajiendesha kisasa siku chache tu zijazo.

Sanga, ambaye kitaaluma ni Injinia, alisema pamoja na ukarabati wa Uwanja wa Kaunda unaoendelea klabuni hapo kwa sasa, wamepanga kufanya mabadiliko katika masuala mengine ya msingi ili kuifanya klabu hiyo kuwa juu.

Bosi huyo wa Yanga, ambaye amepata mafanikio makubwa klabuni hapo akiwa sambamba na bilionea, Yusuf Manji, alisema ukarabati wa uwanja unaendelea vizuri na pia watafanya mabadiliko makubwa katika jengo lao ili kupunguza gharama za uendeshaji.

“Kuna makundi zaidi ya 400 ya mashabiki wa Yanga nchi nzima. Tunataka kuyatumia ili kuibadili klabu. Mashabiki hawa wanaipenda sana Yanga na wapo, suala ni kuwatumia tu katika kuendeleza klabu yetu.

“Mfano tuna vyumba 24 katika jengo la Makao Makuu pale Jangwani, tunaweza kutoa fursa kwa makundi ya Whatsapp kurekebisha vyumba hivyo na kuvipa majina yao ili ifahamike wametoa mchango gani ndani ya klabu.

“Vyumba vinahitaji kuwa na samani nzuri, kuwekwa kwenye hali nzuri na kuwekwa viyoyozi ili viweze kutumika kwa wachezaji,” alisema Sanga na kuongeza: “Kwa upande wa uwanja tayari tumepata vifusi vingi, tunaendelea kupokea vingine. Kuna makundi ya Whatsapp ambayo yamechanga fedha ili kusaidia shughuli hiyo pia, nadhani itakwenda vizuri.

“Wachezaji wa zamani wanasema walipata fedha nyingi kutokana na kiingilio mazoezini, uwanja ukikamilika tunaweza kuweka kiingilio cha Sh 1,000 tu na tukapata fedha nyingi kila wiki ambazo zitasaidia katika kuhudumia klabu,” alisisitiza Sanga.

Alisema kuwa kwa sasa wanatamani kufanya mambo makubwa huku akifichua kuwa, SportPesa walitaka kuipa klabu hiyo basi lakini wametaka wajikite kwenye kuwasaidia kurekebisha uwanja wao ili kuanza kupiga pesa.

Sanga aliongeza kuwa, Yanga ya sasa itaendeshwa kisasa zaidi ili kuhakikisha inakula sahani moja na klabu kubwa barani Afrika kama SuperSports, Mamelodi Sundowns na zingine za Misri ambazo ziko anga za juu kabisa.