Mbwana Samatta awashiwa taa ya kijani

Muktasari:

  • KRC Genk itaanza kuzichanga pointi kwenye kundi lao I, Septemba 20 kwa kucheza dhidi ya Malmö FF ya Sweden kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Luminus.

NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ni kama amewashiwa taa ya kijani baada ya kupangwa kwa ratiba ya Kombe la Europa Ligi kwa kusema ataendelea kupachika mabao ili kuisaidia KRC Genk kuvuka kwenye hatua ya makundi.

KRC Genk itaanza kuzichanga pointi kwenye kundi lao I, Septemba 20 kwa kucheza dhidi ya Malmö FF ya Sweden kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Luminus.

“Kundi letu sio jepesi, tumepangwa na timu ambazo karibu kila msimu zimekuwa zikishiriki michuano hiyo ya Ulaya kwa hiyo tunatambua ugumu uliopo kwenye mechi hizo.

“Nafasi ya kuvuka hatua ya makundi ipo kutokana na kuwa kwetu kwenye kiwango bora kwa sasa. Nataka kufunga karibu kwenye kila mchezo ili kuisaidia timu yangu,” alisema Samatta.

Samatta ambaye amekuwa akitegemewa na Genk kwenye safu yake ya ushambuliaji msimu huu wa 2018/19 amepachika jumla ya mabao tisa kwenye michezo 10, ikiwemo sita ambayo alifunga katika kuwania nafasi ya kutinga makundi.

Hata hivyo, kabla ya Samatta kuiongoza Genk kwenye michezo ya Europa Ligi, mshambuliaji huyo Jumamosi anatarajiwa kuiongoza klabu hiyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji dhidi ya Anderlecht.

Baada ya kucheza na Malmö FF, Genk itasafairi kwa saa moja na dakika 26 kutoka Ubelgiji hadi Norway ambako itacheza ugenini mchezo wake wa pili, Oktoba 4 dhidi ya Sarpsborg 08.

Inaweza kutumia muda huo kama ndege itakuwa inapaa kwa wastani wa spidi ya maili 560 kutoka Ubelgiji kwenda Norway.

Genk itarejea nyumbani kisha kwenda Uturuki ambako itasafiri kwa saa tatu na dakika tatu kwa njia ya ndege inayopaa kwa wastani wa spidi ya maili 560 ili kuutafuta umbali wa maili 1,694 kutoka Ubelgiji hadi Uturuki.

Ikiwa Uturuki itacheza na Beşiktaş anayoichezea beki wa zamani wa Real Madrid, Pepe, Oktoba 25.

Kwa jumla Genk itatumia jumla ya saa nane na dakika 58 kwenye umbali wa maili 4,802 katika safari zao kutoka nchi moja kwenda nyingine pamoja na kurejea Ubelgiji katika mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi.