Mbeya City yala shavu nene

UNAAMBIWA pamoja na kutangazwa kuingia kwenye mfumo wa uendeshaji na sasa kuwa kampuni, Mbeya City itaendelea kuvuna mkwanja wa maana tu kutoka Kampuni ya Coca Cola Kwanza.

Ipo hivi, katikati ya wiki hii Coca Cola kwanza walifanya uzinduzi wa kampeni ya Mzuka Dimbani na Coka maalumu kwa ajili ya Kombe la Dunia na ilifanyikia jijini Mbeya, ndipo mabosi hao wakatoa msimamo wao kuendelea kuibeba City.

Mkurugenzi Mtendaji wa Coca Cola Kwanza, Basic Gadzios alisema wao ni wadau wakubwa wa soka na Mbeya City ni moja ya klabu ambayo imekuwa na uhusiano mzuri.

“Tutaendelea kuiunga mkono Mbeya City, tumekuwa na ushirikiano kwa zaidi ya miaka minne na tutandelea kuimarisha uhusiano huo,” alisema Gadzios.

Katibu Mkuu wa City, Emmanuel Kimbe alisema ni jambo jema kwao kusikia mambo mazuri kutoka kwa wadhamini wao hao huku akiahidi msimu ujao, klabu hiyo itafanya vizuri zaidi kutokana na maandalizi ya maboresho yanayoendelea.