Mbeya City yakomaliachipukizi kuonyesha maajabu

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa timu ya Mbeya City, Ramadhan Nswazurwimo, amefunguka kwamba kikosi chake licha ya kuwa na vijana wengi kitakuwa na utofauti mkubwa katika msimu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akizungumza na MCL Digital, alisema kwamba kikosi chake kina vijana wengi ambao wengine hawajacheza Ligi Kuu kwa muda mrefu, lakini ana Imani na uwezo wa vijana wake.

“Katika kazi yoyote inabidi uwe na malengo tofauti, malengo ya muda mrefu na muda mfupi, naamini kabisa kwamba vijana watanisaidia kwasababu nitakuwa nao kwa muda mrefu hasa hawa wapya wakishirikiana na wenyeji tutafanya vizuri,” alisema.

Akizungumzia maandalizi na changamoto ambazo anakutana nazo katika kipindi hiki cha kujiandaa na Ligi Kuu, alisema kwamba vifaa ndio changamoto kubwa.

“Mechi za kirafiki nazipata na wiki iliyopita nimetoka kucheza Iringa, lakini changamoto ni viwanja ambavyo tunafanyia mazoezi sio vizuri, au hata ukifanya katika uwanja mzuri utaenda kucheza katika uwanja mbaya, hili ni tatizo ambalo linatakiwa liangaliwe kwa ukaribu,” alisema.