Mbeya City yajikita kwa chipukizi

Muktasari:

Gharama kubwa za usajili zimeifanya timu hiyo kutilia mkazo kwa usajili wa wachezaji chipukizi.

Dar es Salaam. Kocha wa Mbeya City, Ramadhan Nsanzurwimo amefichua sababu ya kutoa nafasi kwa kundi kubwa la wachezaji chipukizi katika dakika za lala salama za Ligi Kuu Bara kuwa ni kwa ajili ya kuwaandaa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Nsazurwimo amesema kutokana na gharama kubwa ambazo timu zimekuwa zikipata katika kipindi cha dirisha la usajili, benchi lake la ufundi linaamini njia nzuri ya kuipunguzia timu mzigo ni kutengeneza wachezaji wake na si kusajili kutoka timu nyingine.

"Huwezi kujua kesho timu itakuwa kwenye hali gani kiuchumi kwani dirisha la usajili linaweza kufika na klabu ikawa haina hela ya kutosha kusajili ina maana ndio timu isiwe na wachezaji kwa ajili ya msimu ujao?  Ni lazima kama timu, iwe na vijana wake iliyowaibua na kuwaimarisha ili hata mambo ya kifedha yanaposumbua, tuwe na uhakika wa kuwa na wachezaji bora msimu ujao,"anasema Nsazurwimo.

Ndio maana kwa hizi mechi zilizosalia nimepanga kuwapa nafasi zaidi vijana wanaoonyesha kiwango bora ili waimarike na tuwapandishe moja kwa moja msimu ujao," alifafanua Nsanzurwimo.