Mbeya City, Yanga wala hazichekani

Muktasari:

Binslum aliidhamini Mbeya City kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh360 milioni ambazo alizitoa kwa awamu mbili. Mkataba huo ulikuwa ni wa pili baada ya ule wa awali kumalizika.

HALI mbaya ya uchumi iliyopo ndani ya klabu ya Mbeya City ni mbaya kuliko hata ilivyo kwa wakongwe Yanga na unaambiwa mpaka sasa MCC haijafanya usajili wowote kwa vile haina fedha huku mdhamini mkuu Binslum akimaliza mkataba wake.

Binslum aliidhamini Mbeya City kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh360 milioni ambazo alizitoa kwa awamu mbili.

Mkataba huo ulikuwa ni wa pili baada ya ule wa awali kumalizika.

Yanga nayo hali ya uchumi imeyumba tangu Mwenyekiti wake Yusuf Manji apatwe matatizo yaliyomfanya ajiweke kando na kuifanya klabu ishindwe kufanya makeke ya usajili, kabla ya juzi kumsajili Mohammed Issa ‘Banka’ kutoka Mtibwa Sugar.

Hali inayoendelea ndani ya Mbeya City ambayo ilivuta hisia kubwa za mashabiki wa soka jijini Mbeya na mikoa mingine, imeyumba na kusababisha kushindwa kusajili wachezaji ambao wataisaidia timu hiyo kufanya vizuri msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kama ilivyokuwa msimu wa kwanza ilipopanda daraja kushiriki ligi hiyo.

Nyota kibao wa kikosi hicho wameondoka kwenda kutafuta maisha kwenye timu nyingine baada ya kuona hali ya uchumi inazidi kuporomoka.

Ofisa Habari wa Mbeya City, Shah Mjanja, ameliambia Mwanaspoti mchakato wa usajili unaendelea japo hadi sasa hakuna mchezaji aliyesajiliwa rasmi zaidi ya kufanya nao mazungumzo.