Mbelgiji aleta tiki taka Simba

Muktasari:

  • Pia, Mwanaspoti lilimwanika kocha huyo wakati akiwa jukwaani kuishuhudia Simba ikipepetana na Singida United, ambapo straika wake mpya Meddie Kagere alitupia bao moja matata sana kwenye Kombe la Kagame.

HATIMAYE! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwezi uliopita Mwanaspoti kufichua kuwa, Patrick Asseums, raia wa Ubelgiji ndiye kocha mpya wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba ‘Wekundu wa Msimbazi’.

Pia, Mwanaspoti lilimwanika kocha huyo wakati akiwa jukwaani kuishuhudia Simba ikipepetana na Singida United, ambapo straika wake mpya Meddie Kagere alitupia bao moja matata sana kwenye Kombe la Kagame.

Sasa ni rasmi kuwa Asseums anabeba mikoba ya Mfaransa Pierre Lechantre, ambaye aliingoza timu hiyo kubeba ubingwa wa kwanza baada ya misimu mitano bila taji hilo.

Sasa jana mabosi wa Simba wakiongozwa na Kaimu Rais, Salim Abdalah ‘Try Again’ wakamtambulisha kwa mashabiki na wapenzi wa Simba na amesaini mkataba wa mwaka mmoja akiwa na kibarua cha kutetea ubingwa huo na kuipaisha Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Achana na kutambulishwa kwake, ishu ni idadi ya makocha ambao waliomba kibarua cha kuinoa Simba, lakini mara paap Asseums akalamba dili hilo. Imefichuliwa kuwa makocha 57 wakiwemo wazawa na wale wa kimataifa walituma maombi ya kazi hiyo, lakini mwisho wa siku Mbelgiji huyo akaonekana ni zaidi ya wengine.

Kuonyesha Simba haikukosea kumpa kazi beki huyo wa zamani wa ES Toyes ya Ufaransa, ametoa picha kuwa kikosi chake kitakuwa cha kazi mwanzo mwisho na wale wachezaji waliozoea kubembelezwa itakula kwao.

ALIVYOPATIKANA

Katika mkutano huo jana, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alieleza kuwa makocha 57 walioomba kazi hiyo ambapo jopo la wataalamu na wadau wa soka wakiongozwa na Mkufunzi wa Fifa, Sunday Kayuni, ndio walikuwa na jukumu la kuwahoji na baadaye kumpitisha mmoja.

“Kocha huyu ni wa tofauti kabisa kwani, hata kupatikana kwake kulizingatia mambo mengi. Wataalamu wakiongozwa na Kayuni, Salum Madadi, Mshindo Msolla, kocha wa timu ya Taifa ya Vijana ndio walimhoji uwezo wake kwa takribani saa tano,” alisema.

Alisema kuwa katika mahojiano yake, wataalamu hao walijiridhisha kuwa Asseums ni kocha wa kiwango cha juu na anafahamu kazi yake kikamilifu.

AFUNGUKA ISHU NZIMA SIMBA

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Asseums alisema alikuwa na ofa nyingi kutoka timu za Afrika, lakini aliona Simba kunaweza kuwa sehemu muafaka baada ya kufanya mazungumzo na Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji (MO).

“Ndio, nimeamua kuja hapa baada ya kuzungumza na Dewji kwa kina na akanieleza mipango yake kuwa anataka Simba kuwa klabu kubwa Afrika. Nina uzoefu wa kutosha hivyo, nauleta hapa kwa ajili ya kutimiza malengo hayo,” alisema.

Patrick aliongeza kuwa anafahamu Simba ni klabu kubwa nchini lakini, dhamira yake ni kuifanya kuwa tishio barani Afrika.

“Najua Simba hapa iko juu, ila lengo langu ni kuhakikisha inaendelea kuwa juu Afrika, watu wazidi kuielewa,” alisema.

STAILI YA SOKA LAKE

Soka la Lechantre lilikuwa na kukaba zaidi na kutengeneza nafasi chache za mabao, lakini hapa kwa Mbelgiji mambo ni tofauti kabisa unaambiwa. Jamaa anakuja na soka tofauti kabisa akionekana kuwa staili ya tiki taka kama ya Pep Guardiola wa Man City ambapo bao ni lazima zipigwe pasi zaidi ya 10.

Ameweka bayana kwamba hataki soka la Kiingereza la pasi mbili wako golini wanafunga na kama wachezaji watashindwa kwenda na staili hiyo basi watapata tabu sana.

“Kila mwalimu ana falsafa yake ya ufundishaji, timu yangu nataka imiliki mpira na kucheza soka la utulivu, sitaki wanapiga pasi mbili wako golini kwa wapinzani wanafunga bao, hapana hiyo staili yangu kabisa,” alisema.

Pia, alifichua kuwa anapenda kuwa kwenye timu ambayo wachezaji wake wanakuwa na furaha uwanjani kwa kuwa itasaidia kuwapa morali.

AWATAJA BOCCO, OKWI, KICHUYA

Msimu uliopita mastaa wa Simba; Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya walikuwa kwenye wakati mzuri kwelikweli. Huwezi kutaja mafanikio ya Simba bila kuwataja na hilo linathibitishwa na Aussems, ambaye amekiri kuwa anawafahamu sana hao jamaa.

Alisema amekuwa akiifuatilia Simba kwa muda mrefu hivyo Bocco, Okwi na Kichuya anawatambua sana tu.

“Nimetazama mikanda ya Simba katika mechi za ligi na ile ya kimataifa dhidi ya Al Masry, naweza kusema naifahamu vizuri na hata wachezaji wake naamini nitafanya nao kazi vizuri,” alisema.

Pia, anafahamu ushindani uliopo katika Ligi Kuu Bara na hasa kwa timu za Yanga na Azam, lakini anaanza kwa kuiangalia timu yake ili iweze kufanya vizuri.

“Najua kuna ushindani hapa lakini hao kwanza siwaangalii, kikubwa nataka timu yangu ifanye vizuri ili nikikutana nao we tupo vizuri zaidi yao,” alisema.

MASHARTI YA USAJILI MPYA SIMBA

Kama una ndoto za kukipiga Simba ni lazima ujipange kwelikweli kwani, kama ni mchezaji wa kigeni na hujawahi kuwa na timu iliyoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ama Kombe la Shirikisho au haupo kwenye timu ya Taifa basi huwezi kusajiliwa Simba.

Msikie mwenyewe Try Again hapa: “Kocha anatuambia tu kuwa anataka mshambuliaji mrefu au mwenye umbo fulani kisha tunatafuta aina hiyo na kumsajili, lakini hatusajili bila mapendekezo yake.

“Tunaweza kusajili mchezaji yeyote kutoka nje ya nchi, lakini vigezo vyetu kama ni mchezaji wa kigeni ni lazima uwepo kwenye timu ya taifa ya nchi yako ama uwe katika klabu iliyopo kwenye michuano ya Afrika. Tofauti na hapo huna nafasi Simba.”

KUMBE PIERRE KAJIKABA TU

Mashabiki wengi wa Simba wanaamini mabosi wa Simba walimfyeka Lechantre, lakini Try Again kafunguka ishu nzima ilivyokuwa. Amesema kuwa Mfaransa huyo alikuwa na ofa kibao mezani hivyo, wasingeweza kumpa kazi kwani hakuwa amejiandaa kubaki.

“Alimaliza mkataba na Simba na tulijiandaa kuanza mazungumzo ya mkataba mpya, lakini tukaona ameomba kazi kuifundisha timu ya Taifa Cameroon na alikuwa katika hatua nzuri ya kuipata. Sasa tunafanyaje kazi na mtu wa aina hii, anaweza kutuacha muda wowote hivyo, tukaona tuachane naye,” alisema.

Pia, amefichua Asseums amemkubali Masoud Djuma na wataendelea kufanya kazi pamoja tofauti na makocha wengine ambao, huweka sharti la kuajiriwa kwa wasaidizi wanaokuja nao.

“Aussems hakutaka kuja na Kocha Msaidizi, ametaka kufanya kazi na kocha mzawa ama kutoka ukanda wa Afrika, ambaye analijua vyema soka kama ilivyo kwa Masoud ili iwe rahisi kushauriana. Kwa sasa tunahitaji kocha wa viungo tu,” alisema.