Mbaya wa Nigeria kuzihukumu England, Croatia

Muktasari:

Cuneyt Cakir raia wa Uturuki, anatajwa kuwa mmoja wa waamuzi wenye msimamo na amekuwa akipewa lawama lukuki kutokana na uamuzi wake.

Moscow, Russia. Mwamuzi mwenye uamuzi uliogubikwa na utata, amepangwa kupuliza filimbi katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia baina ya England na Croatia.

Cuneyt Cakir raia wa Uturuki, anatajwa kuwa mmoja wa waamuzi wenye msimamo na amekuwa akipewa lawama lukuki kutokana na uamuzi wake.

Mwamuzi huyo mwenye miaka 41, ndiye aliyeinyima Nigeria mkwaju wa penalti katika mchezo ambao timu hiyo ilichapwa na Argentina.

Beki wa kati Marcos Rojo alishika mpira ndani ya eneo la hatari, lakini mwamuzi huyo alipeta licha ya kulalamikiwa na wachezaji wa Nigeria wakiongozwa na Mikel Obi.

Cakir alipuliza filimbi katika mchezo ambao Iran iliichapa Morocco bao 1-0 kabla ya Argentina kuilaza Nigeria mabao 2-1.

Katika mechi zote mbili alizochezesha, mwamuzi huyo aliweka rekodi ya kutoa jumla ya kadi tisa za njano na alilalamikiwa sana na Nigeria kwa uamuzi usiofaa.

Tukio la Nigeria kunyimwa penalti licha ya mwamuzi huyo kuona tukio hilo liliibua mjadala mzito kwa wadau wa soka waliohoji uwezo wake wa kusimamia sheria 17.

“Nashindwa kumwelewa mwamuzi huyu, alikwenda kuangalia tukio katika VAR, lakini alitunyima haki. Nilimuuliza ameshika akanijibu ndiyo. Lakini kwanini isiwe penalti alijibu hajui,” alisema Mikel.

Cakir, mwenye uzoefu wa miaka 17, alisimamia mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014 baina ya Uholanzi na Argentina.

Mwamuzi huyo anakumbukwa na mashabiki wa Chelsea, baada ya kumpa kadi nyekundu aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho John Terry, katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona mwaka 2012.