Mbaya wa Azam amerudi

Muktasari:

  • Mtibwa na Azam zinatarajiwa kuvaana katika robo fainali unaotarajiwa kuwa mkali kutokana na upinzani wa timu hizo ambazo zilishindwa kutambiana kwenye mechi yao ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex.

STRAIKA wa Mtibwa Sugar, Kelvin Sabato ‘Kiduku’ aliyekuwa majeruhi tangu duru la kwanza la Ligi Kuu Bara, amerejea uwanjani na tayari ameungana na wenzake kuisubiri Azam katika mechi ya Kombe la FA.

Mtibwa na Azam zinatarajiwa kuvaana katika robo fainali unaotarajiwa kuwa mkali kutokana na upinzani wa timu hizo ambazo zilishindwa kutambiana kwenye mechi yao ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex.

Katika mchezo huo, Kiduku ndiye aliyefunga bao kali la kusawazisha kwa kupiga faulo kali nje ya eneo la hatari na kumuacha kipa bora kwa wakati huo Razak Abarola akishangaa tu.

“Nimerudi na nipo kambini tena fiti kabisa nafanya mazoezi na wenzangu na nahamu kubwa ya kuludi uwanjani kwani nimekosa mechi nyingi ambazo zimechangia kufuta ndoto zangu za kufunga magoli zaidi ya msimu uliopita.”

“Kama kocha akinipa nafasi ya kucheza mechi ya Azam itakuwa fursa tena kwangu kwani kuifunga timu kwa mara ya pili mfululizo unaongeza thamani yangu kama mchezaji,” alisema Kiduku aliyefunga mabao 10 msimu uliopita.