Mbappe ni hatari kuliko Ronaldo na Messi

Muktasari:

Mbappe mpaka sasa amefunga mabao 52 akiwa amezichezea klabu za Monaco huku takwimu zikionyesha kuwa katika umri huo, Messi akiwa na Barcelona alikuwa amefunga mabao 25 wakati Ronaldo akiwa na Manchester United alikuwa amefunga mabao 17 tu.

PARIS, UFARANSA. Mwanadamu anaweza kudanganya lakini namba hazidanganyi. Hazidanganyi kamwe. Na sasa imebainika kwamba kinda wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe ni tishio kuliko mastaa wawili wanaotamba duniani kwa sasa, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Kwa mujibu wa takwimu, katika umri wa miaka 19, kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 ambaye ametoka kuchukua kombe la dunia na Ufaransa nchini Russia amefanya mambo makubwa kuliko ambayo Ronaldo na Messi walifanya wakiwa na umri huo.

Mbappe mpaka sasa amefunga mabao 52 akiwa amezichezea klabu za Monaco huku takwimu zikionyesha kuwa katika umri huo, Messi akiwa na Barcelona alikuwa amefunga mabao 25 wakati Ronaldo akiwa na Manchester United alikuwa amefunga mabao 17 tu.

Kama vile haitoshi, tayari Mbappe amefunga mabao mengi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika umri wake kuliko Ronaldo na Messi. Wakati Mbappe ana mabao 10 mpaka sasa katika michuano hiyo, katika umri wake Ronaldo alikuwa hajafunga bao lolote la michuano hiyo wakati Messi alikuwa amefunga mabao mawili tu.

Mbappe ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji kijana zaidi kuifungia Ufaransa katika michuano ya kombe la dunia pia anasimama mbele ya mastaa hao wawili kwa kuifungia timu yake ya taifa mabao mengi zaidi akiwa katika umri huo.

Mpaka sasa Mbappe ambaye alikuwa mshambuliaji namba moja wa Ufaransa Russia ameifungia Ufaransa mabao 10 wakati katika umri huo Ronaldo alikuwa ameifungia Ureno mabao saba huku Messi akiwa ameifungia Argentina mabao manne tu.

Katika umri wa miaka 19 tayari Mbappe amekuwa mchezaji wa pili mdogo katika historia kufunga bao katika fainali ya kombe la dunia baada ya mfalme wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’ ambaye alifunga bao katika fainali za mwaka 1958 dhidi ya Sweden akiwa na umri wa miaka 18.

Mbappe tayari ameshachukua kombe la dunia akiwa na umri wa miaka 19 tu wakati katika umri huo Messi aliichezea Argentina katika pambano la kombe la dunia mwaka 2006 dhidi ya Mexico nchini Ujerumani.

Kwa ujumla katika michuano hiyo Messi alicheza mechi tatu kati ya tano za Argentina katika michuano hiyo. Hata hivyo Messi aliingia katika michuano hiyo akiwa tayari ameshachukua mataji mawili ya La Liga na moja la Ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Wakati huo huo katika umri huo Ronaldo aliichezea timu ya taifa ya Ureno katika michuano ya Euro 2004 iliyofanyika nchini kwao Ureno. Alicheza mechi sita huku akianza mechi nne na mechi mbili akitokea katika benchi.

Katika michuano hiyo ambayo Ureno ilichapwa pambano la fainali na Ugiriki Ronaldo alifunga bao lake la kwanza kwa kikosi cha Ureno. Katika michuano ya ndani alikuwa amecheza msimu mmoja na Manchester United katika Ligi Kuu ya England.

Mbappe kama ilivyo Messi amekwenda katika michuano ya kombe la dunia nchini Russia mwaka huu akiwa ana mataji mawili kibindoni. Moja likiwa na timu yake ya zamani Monaco wakati jingine likiwa na PSG msimu uliopita.

Mbappe alizaliwa katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris huku Baba yake akiwa ni mzamiaji kutoka Cameroon, Wilfriend Mbappe wakati Mama yake, Fayza Lamari  yake ana asili ya Algeria. Baba yake pia amekuwa akifanya kazi kama wakala wake.

Mdogo wake Mbappe, Ethan Mbappe anakipiga katika timu ya watoto ya PSG  chini ya umri wa miaka 12 na amekuwa akionekana na Mbappe katika maeneo mbalimbali nchini kwao Ufaransa. Shujaa wa Mbappe utotoni Cristiano Ronaldo.