Mbao yaibana Sony Sugar ya Kenya

Thursday July 27 2017

 

By THOMAS NG’ITU

Timu ya Mbao FC imetoshana nguvu na klabu ya Sony Sugar ya nchini Kenya katika mchezo wa kirafiki uliopigwa mkoani Mara baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ikiwa ni maaandalizi kwa vilabu hivyo kujiweka fiti na kuwapima wachezaji wao waliowasajili.

Mratibu wa timu hiyo, Masalinda Njashi alisema waliamua kuitafutia timu yao mechi za kirafiki za kimataifa, kwa sababu timu yao ina vijana wengi wapya ambao wengine hawakuwahi kushiriki katika ligi hivyo wanawapa ujasiri wa mapema.

“Timu yetu ya hivi sasa ina vijana wengine ambao ni wapya kabisa ambao wamechanganyika na wale wa zamani, sasa ukienda moja kwa moja katika ligi bila kuwatengenezea kujiamini, italeta shida kwa hiyo tumeona bora tuanze na mechi za kirafiki za kimataifa,”alisema.

Akizungumzia usajili wao walioufanya alisema kuwa klabu yao ilikuwa ikiendesha programu maalumu ya kutafuta vijana kwa ajili ya kutumikia vikosi vyao hivyo kwa vijana ambao wamechaguliwa na mwalimu wao siyo rahisi kuwaacha.

“Hatuna pesa kubwa sisi ya kufanya usajili lakini tuliendesha programu ambayo imesaidia timu kwa namna moja ama nyingine kutokana na wachezaji wote ambao tumewasajili waliotokana na programu yetu. Siwezi kusema tumefunga usajili kwasasa kwasababu vijana walikuwa wengi hivyo tunasubili mrejesho wa mwalimu kuangalia kuwa wapi watakuwa timu ya wakubwa na wapi timu ndogo japokuwa mpaka hivi sasa baadhi ya wanaotakiwa timu kubwa tumemalizana nao,”alisema.