Mayanga atetea uamuzi wake Taifa Stars

Tuesday November 14 2017

 

By DORIS MALIYAGA

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, amefafanua sababu ya kumchezesha kiungo, Himid Mao katika nafasi ya beki wa kulia, akisema ni mbinu za kiufundi na akaweka wazi timu anayoihitaji imeanza kukaa kwenye mstari.

Mayanga alimtumia Himid kucheza nafasi hiyo katika mechi yao dhidi ya Benin ambayo walimaliza kwa sare ya bao 1-1, mechi iliyochezwa Jumapili iliyopita.

Amesema aliona Himid ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo kwa sababu kwake si ngeni, hata Azam huwa anaicheza.

“Niliona Himid ni mtu sahihi kucheza nafasi hiyo, si mara ya kwanza, amekuwa akicheza nafasi hiyo kwa vipindi tofauti akiwa na klabu yake ya Azam namjua na ndiyo maana, nikafanya maamuzi hayo,” alisema Mayanga ambaye alichukua uamuzi huo baada ya Erasto Nyoni kuwa nje akitumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Mayanga ambaye tangu aanze kuinoa Stars, amekuwa na matokeo ya ushindi mwembamba au sare ambayo mwenyewe huyafafanua yanatokana na mbinu zake zake na ndiyo maana hafungwi.

Na lengo lake kuwa ni kuiimarisha timu isifungwe kabisa na huku akirekebisha katika ushambuliaji ili apate idadi kubwa ya mabao.

Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mchezo huo wa kirafiki, Mayanga alisema: “Kwa ujumla timu iko vizuri na imecheza kwa kiwango chake.

“Kwangu ni nafasi nzuri na sasa nimeanza kuiona timu imara niliyokuwa naihitaji.

“Cha muhimu Watanzania watulie tuendelee kuijenga timu kwa faida ya nchi, mwenendo unaridhisha.”