Taifa Stars yauvaa muziki wa Algeria

Dar es Salaam. Kocha anayemaliza muda wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameamua kujilipua kwa kucheza soka la kushambulia dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Juillet, Algiers leo saa 2:00 usiku.

Katika mchezo huo kocha Mayanga ameingia na mfumo wa 4-3-3 wakati wapinzani wake Algeria wenyewe watakuwa wakicheza 3-5-2.

Katika mfumo huo, Mayanga amewapa Himid Mao na Mudathir Yahaya jukumu la kulinda zaidi pamoja na mabeki Gadiel Michael, Shomari Kapombe, Abdi Banda na Kelvin Yondani.

Wakati Said Ndemla atakuwa akicheza chini ya washambuliaji watatu Shiza Kichuya, Saimon Msuva na nahodha Mbwana Samatta.

Kikosi hicho kilichoanza kitakuwa ni bora zaidi wakati Stars itakapokuwa inamiliki mpira na kushambulia, lakini watakapokuwa wamepoteza mpira hali itakuwa mbaya.

Kosa kubwa kwa Mayanga ambaye tayari TFF imetangaza kuanza kwa mchakato wakutafuta kocha wa kumrithi ni kutaka kupishana na Algeria.

Pamoja na kuwa ni mchezo wa kirafiki bado Mayanga alitakiwa kupunguza idadi ya mabao kwa kucheza kwa kulinda zaidi kwa kuongeza idadi ya viungo wakabaji.

Mabeki wake wapembeni Gadiel Michael na Kapombe ni mchezaji wanaopenda kushambulia wakati mawinga Kichuya na Msuva si wazuri katika kusaidia kulinda jambo hilo litakuwa hatari zaidi wakati Algeria itapokuwa ikifanya mashambulizi ya kushtukiza.

Kutokana na mfumo huo Mao na Mudathir watalazimika kufanya kazi ya kuwazuia viungo wa Algeria Yacine Brahimi (FC Porto), Riyad Mahrez (Leicester City), Nabil Bentaleb (Schalke 04), Ismael Bennacer (Empoli), Zinedine Ferhat (Le Havre).

Ndemla hatokuwa na msaada kwa timu hiyo katika kulinda kwa sababu yeye kwa asili ni kiungo mshambuliaji ndiyo maana kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre kutomtumia katika mechi dhidi ya Al Masry.

Mayanga baada ya kuwa na Kichuya na Msuva pamoja na Michael na Kapombe katika kushambulia alipaswa kumuanzisha Erasto Nyoni badala ya Ndemla unapocheza dhidi ya timu bora inayosifika kwa kucheza soka la kushambulia barani Afrika.

Kocha wa timu ya taifa ya Algeria, Rabah Madjer ameweka bayana lengo la mechi hiyo ni kuangalia jinsi vijana wake walivyoelewa mbinu zake, pia kuangalia jinsi kila moja atakavyoonyesha uwezo wake kuelekea katika mechi zao za kusaka kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika.

Taifa Stars na Algeria zimekutana mara tisa tangu 1973 katika mashindano mbalimbali, Tanzania ikishinda mechi mmoja 1995,  wakifungwa mechi nne na kutoka sare mara nne.

Stars ilishinda 2-1 dhidi ya Algeria Januari 1995 ukiwa ni ushindi pekee katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika.

Hata hivyo, Taifa Stars ipo Algeria wakiwa na kumbukumbu ya kunyukwa mabao 7-0, Novemba 2015 wakati wa mechi ya kusaka kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018.

Algeria kwa sasa ipo nafasi 60 katika orodha ya viwango vya ubora wa Fifa wakati Tanzania ikiwa nafasi ya 146 iwapo Tanzania itashinda itapanda zaidi katika orodha hiyo ya Fifa.

Baada ya mechi hiyo, Stars itarejea nchini kujiandaa na mechi nyingine ngumu zaidi dhidi ya DR Congo iliyo nafasi ya 39, katika orodha ya ubora wa Fifa Machi 27.

Taifa Stars na DR Congo wamekutana mara tano tangu 1995, mara mbili katika mechi za mashindano na mara tatu katika michezo ya kirafiki.

Tanzania imeshinda mechi mara mbili, sare moja na kufungwa mechi mbili mara ya mwisho zilipokutana Februari 23, 2012 timu hizo zilitoka suluhu.

 

Kikosi cha Stars:

Mohamed Abdulrahman, Gadiel Michael, Shomari Kapombe, Abdi Banda, Kelvin Yondani, Himid Mao, Mudathir Yahya, Said Ndemla, Shiza Kichuya, Saimon Msuva na Mbwana Samatta.