Matano yaliyojiri msiba wa Majuto

AGOSTI 10, ndiyo iliyokuwa hitimisho la safari ya duniani ya aliyekuwa gwiji wa vichekesho nchini, Amri Athuman ‘King Majuto’.

Siku hiyo ndio mwili wa gwiji huyo ulipoingizwa katika nyumba yake ya milele baada ya miaka 70 ya uhai wake duniani. King Majuto alifariki dunia usiku wa Jumatano iliyopita jijini Dar.

Majuto alizikwa shambani kwake kijijini Kiruku, jijini Tanga, ambapo viongozi wa serikali, wasanii, ndugu, jamaa na marafiki walishiriki katika kuhimitisha safari yake hiyo ndefu.

Lakini katika msiba huo, kuna mambo mengi yalijitokeza mara tu mwili wa marehemu ulipofikishwa nyumbani kwake Donge hadi akipoenda kuzikwa Kiruku.

Kutoka Donge hadi shambani Kiruku alipozikwa Majuto ni kama umbali wa kilometa 20 na Mwanaspoti iliyosafiri mpaka kijijini humo inakumegea mambo hayo matano.

KUJITENGA KWA WASANII

Hakuna siri kwamba waigizaji wa filamu na wachekeshaji hasa wa kike wamekuwa wakitegana kwenye shughuli mbalimbali bila ya sababu.

Hata kwenye msiba wa Majuto, hali ilikuwa hivyo. Hii haikuwa sawa kwani mastaa hao walionyesha kujitofautisha kisanaa mara baada ya kutua Tanga.

Wasanii hao walikaa makundi mawili, moja la waigizaji wa filamu na jingine la wachekeshaji jambo ambalo lilifanya baadhi ya waombolezaji kubaki na maswali lukuki vichwani.

Wasanii wa kike wa filamu waliojiwekwa kivyao ni Irene Uwoya, Shamsa Ford, Sango Matrida, Kajala Masanja, Mariam Ismail, huku wachekesaji wakiwa na kundi lao chini ya Tausi, Matumaini, Asha Boko, Rehema Majuto na wengine.

MWILI KUTOLEWA MAPEMA JENEZANI

Kwa hali ya kawaida mtu hawezi kuamini kitendo hiki, ila ndio ukweli ulivyo. Mwili wa Mzee Majuto ulitolewa katika jeneza hata kabla ya kufika makaburini kuzikwa.

Ilikuwa hivi: Kutoka Donge jijini Tanga hadi kufika mahala alipozikwa Mzee Majuto, yaani Kijiji cha Kiruku ni umbali wa kilometa 20, hivyo basi huku mwili ukisaliwa Msikitini wakazi wa Tanga walianza kujipanga barabarani kwa ajili ya kwenda kuzika.

Walipokuwa wanaenda kuzika, karibu ya kufika makaburini watu walianza kugombania mwili kila mtu akitaka kuushika na matokeo yake jeneza likavunjika na mwili huo ulitolewa.

WAKAZI TANGA WAWAZINGUA WASANII

Wakazi wa Tanga licha ya sifa kubwa ya ukarimu na upendo waliyonayo, kwenye msiba huo wa Majuto walionyesha mambo yanayoweza kutafsiriwa kama ulimbukeni flani hivi.

Unajua nini? Baadhi yao walikuwa kila wakimuona msanii walimvamia kwa kumvutavuta huku makelele ya shangwe zikirindima.

Haikufahamika ilitokana na nini awali, lakini baadaye ilikuja kubainika kuwa walipagawa kwa kutowahi kuwaona laivu wasanii hao na kujisahau kama wapo msibani.

Kitendo cha wakazi hao kiligeuka kuwa kero kwa wasanii hadi walishindwa kutoka nje kwa waliokuwa ndani na baadhi yao kushindwa hata kwenda kuchukua chakula na badala yake kupelekewa ndani kwa kuwakwepa wasumbufu hao.

Kuna wakati walipokuwa wakishangilia walisahau kama ule ni msiba na matokeo yake wakawa wanaonyesha furaha kupita kiasi huku wakiwashangilia kwa kuwataja majina yao.

Wasani waliopatwa maswahibu hayo ni; Harmonize, Yusuf Mlela, Hemed PHD, JB, Irene Uwoya, Shamsha Ford, Steve Nyerere, Dude,Cloud 112, Mboto na Nisha.

UZUSHI WATAWALA MSIBANI

Wakazi wa Tanga waliohudhuria msiba huo, walikuwa wakinong’ona chini kwa chini eti wakidai kuwa gwiji huyo kifo chake kimetokana na mambo ya kishirikina.

Kisa cha kuzusha tuhuma hizo, eti ni jinsi marehemu alivyoteseka akifanyiwa upasuaji mara mbili kabla ya kuzidiwa na kufariki, bila kujua kila nafsi huonja mauti.

Tuhuma ziliibuka tangu baada ya Julai 31, 2018 Majuto alipozidiwa na kupelekwa hospitalini na mtoto wake Ashrafu, ambaye alitoa majibu kuwa mzee wake amepimwa vipimo vyote hakuonekana na ugonjwa wowote.

Hapo ndipo mambo yakaanza kwa madai kuwa hakuna kitu kingine ila mambo ya ndumba tu.

Pia walidai alifanyiwa upasuaji mara mbili ya kwanza ukiwa ni wa ngiri na mwingine wa tezi dume na kuhoji, mbona wa tezi dume ulimsaidia ila wa ngiri ulishindwa kumpa nafuu na ndipo wakazusha.

Hata familia imeeleza ukweli kuwa marehemu amefariki kwa maradhi yaliyoelezwa na juhudi za madaktari zilifikia mwisho na nguvu ya Mungu ikachukua nafasi yake.

WENGI WASHINDWA KUMZIKA

Japo idadi ya watu waliofika makaburini kumzika Majuto ilikuwa kubwa, lakini walioshindwa kushiriki ibada hiyo walikuwa kwengi kwelikweli.

Hii ilitokana na wingi wa watu na kufanya waliokuwa mbali na makaburini kuamua kugeuza kurudi makwao.

Kwani njia ya kuelekea makaburini ilikuwa haipitiki na hata baadhi ya waandishi wengi wao walishindwa kufika katika eneo hilo kuchukua matukio kwa kukosekana nafasi ya kupita.

Kuna baadhi kwa kutotaka kupitwa na tukio la kuhifadhiwa kwa mwili wa marehemu katika nyumba yake ya milele, walilazimika kuparamia miti, hii ikionyesha namna gani msiba wa King Majuto uliwagusa wengi.

Marehemu aliyezaliwa mwaka 1948 na kuanza kuigiza miaka 10 baadaye atakumbukwa kwa ucheshi wake na jinsi alivyokuwa mahiri katika kuvunja wavu mbavu na ushirikiano wake na wasanii wenzake bila kujali umri, jinsia ama rangi.