Mastraika Alliance Queens pasua kichwa

JAMAA kashindwa kujizuia. Kocha wa Alliance Queens, Ezekiel Chobanka amesema kuwa kwa kipindi hiki Ligi Kuu ya Wanawake ikiwa imesimama, atatumia muda mwingi kurekebisha mapungufu ya safu yake ya ushambuliaji iliyomwangusha kwa sasa.

Timu hiyo ya jijini hapa, imevuna pointi saba na ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi hiyo inayoongozwa na vinara JKT Queen wenye alama 12, kila moja ikicheza mechi nne mpaka sasa.

Kocha Chobanka alisema katika kuhakikisha wanawania ubingwa, atapambana kwa nguvu kuisuka vyema safu ya ya mbele ili kila mchezo wapate mabao ya kutosha.

Alisema kuwa licha ya mapungufu mengine yaliyopo kama eneo la beki, lakini mastraika wamemuangusha na hivyo anahitaji kuwaweka sawa ili wawe wanamalizia nafasi wanazotengeneza na kuipaisha timu yao.

“Ushindi wowote huwa ni mabao, hata hao JKT wanaoongoza ni kwa vilewalishinda kwa kufunga mabao, hivyo nami kwa muda huu nitahakikisha safu ya ushambuliaji inakaa sawa,” alisema Chobanka.

Aliongeza matarajio yake ni kuisaidia timu hiyo kubeba ubingwa na kwamba uwezo wa vijana wake ndio unampa kiburi cha kutamba kufanya kweli.

Alisema licha ya ushindani uliopo kwa timu pinzani, lakini hana wasiwasi na kwamba lazima awashushe JKT na Kigoma Sisterz zilizopo juu yao kwenye msimamo wa ligi hiyo.