Mastaa wa Yanga washituka mapema

MASTAA wa Yanga,wameapa  kufika hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho,wakitaka kutumia vizuri  Uwanja wa Taifa,jijini Dar es Salaam.
Yanga itacheza na Welayta Dicha ya Ethiopia  baada ya kutolewa klabu bingwa Afrika na Township Rollers ya Botswana.
Mabeki wa timu hiyo,Haji Mwinyi na Hassan Kessy,wamezungumza kwa nyakati,kuelezea matumaini ya kufika hatua ya makundi,wakisisitiza kupata ushindi uwanja wao nyumbani ndio utakaowapa hatua.
"Kitendo cha kutolewa kirahisi na Township Rollers,kimetufunza faida za kushinda nyumbani,ili ugenini tuwe tunajilinda,kiufundi uwanjani sioni walichotuzidi kwa timu ambazo tumecheza nazo," alisema.
"Ili tufike mbali,tunahitaji nidhamu ya hali ya juu ya kimchezo,tunaanzia nyumbani hii ni fursa nyingine kwetu,lazima tuamke usingizini na tusimame kwa ajili ya kupigania taifa letu,sisi ndio tumebaki kuiwakilisha nchi,"alisema.
Kwa upande wa washambuliaji,Emmanuel Martin na Yohana Mkomola, walisema mabao mengi ya nyumbani ndio yatakayowaweka salama ugenini.
"Tunatakiwa kujipanga na kufunga mabao mengi nyumbani,ili tukifika ugenini,tuwe tunashambulia kwa kushitukiza,naamini tutapiga hatua,"alisema Martin.
"Hata kama timu tunayocheza nayo hatuijui,kikubwa ni maandalizi ya nguvu,tuhamasishane ili kurahisisha kazi nyumbani,ugenini iwe kutunza ushindi,"alisema Mkomola.
Nyota wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa ni kocha wa timu B, aliwashauri nyota wa Yanga,kwamba wanatakiwa kucheza kwa utulivu,nidhamu,kujituma na uzalendo ambapo anaamini watafika mbali.
"Tayari Yanga na Simba, zimeishapata funzo namna ambavyo walicheza mechi za kwanza walizotolewa,umakini wao utawafanya wafike mbali michuano ya shirikisho,"alisema.